Tanzania, Saudi Arabia zaimarisha ushirikiano wa elimu

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 05:09 PM Dec 11 2025
Tanzania, Saudi Arabia zaimarisha ushirikiano wa elimu
Picha: Mpigapicha Wetu
Tanzania, Saudi Arabia zaimarisha ushirikiano wa elimu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amekutana na Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Yahya Bin Ahmed Okeish, kwa mazungumzo yenye lengo la kuimarisha sekta ya elimu na kupanua fursa za ufadhili wa masomo kwa vijana wa Kitanzania.

Mazungumzo hayo yalifanyika Desemba 11, 2025, jijini Dar es Salaam, ambapo Prof. Mkenda ameishukuru Serikali ya Saudi Arabia kwa kuongeza nafasi za ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kutoka 90 hadi 127 kwa Watanzania. Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha fursa hizo zinatumika kikamilifu ili kuwawezesha vijana kupata elimu bora katika vyuo na taasisi mbalimbali nchini Saudi Arabia.

Amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuimarisha mfumo wa elimu kupitia maboresho ya kimkakati katika maeneo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Sayansi ya Takwimu na Akili Bandia, ili kuwajengea vijana ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake, Balozi Okeish amesema Saudi Arabia inajivunia uhusiano wake na Tanzania katika kukuza elimu na ameahidi kuendeleza ushirikiano huo kwa kuunga mkono mikakati ya kukuza ujuzi wa vijana wa Kitanzania, hususan katika maeneo yenye kipaumbele cha kitaifa.

Aidha, ameipongeza Wizara ya Elimu kwa kuwa na Sera ya Elimu iliyo bora pamoja na mipango ya kufanya ziara nchini Saudi Arabia kutembelea vyuo mbalimbali, kubadilishana uzoefu na kupanua fursa za elimu kwa vijana wa mataifa hayo mawili. Pia ameahidi kuunga mkono mpango wa kuimarisha ufundishaji wa lugha ya Kiarabu nchini.