Mabilioni yawekezwa kuwezesha mradi wa umeme jua Zambia

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:50 PM Dec 11 2025
news
Picha Mpigapicha Wetu
Mabilioni yawekezwa kuwezesha mradi wa umeme jua Zambia

KAMPUNI ya Tanzania ya Amsons pamoja na nyingine ya nishati barani Afrika, yameanza ushirikiano wa kimkakati na kampuni ya 'Exergy Africa Limited' ya Zambia kujenga na kupanua miradi ya uzalishaji na miundombinu ya nishati nchini humo.

Mradi huo utahusisha megawati 1,000 za umeme wa jua na 300 za umeme wa makaa ya mawe, kwa uwekezaji wa jumla wa Dola za Marekani milioni 900 ambapo Dola milioni 600 ni kwa ajili ya umeme jua na 300 kwa ajili ya makaa ya mawe.

Makubaliano hayo ambayo ni sehemu ya mkakati wa Amsons wa kupanua biashara katika sekta ya nishati, yanajumuisha uwekezaji katika kituo kikubwa cha umeme wa jua chenye uwezo wa Gigawati moja (sawa na megawati 1,000) kupitia 'Africa Power Generation' muunganiko wa wawekezaji wa nishati jadidifu uliosajiliwa Zambia.

Hafla ya kutiwa saini ya ushirikiano huo ilifanyika Ikulu ya Zambia hivi karibuni, na kuongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Amsons Group, Edha Nahdi, chini ya uwepo wa Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, ambaye alisisitiza umuhimu wa uwekezaji huo katika kuongeza usalama na mseto wa nishati nchini humo.

“Uwekezaji huu wa Gigawati moja ni mabadiliko makubwa. Unakabili moja kwa moja uhaba wa nishati nchini kwa kutoa umeme wa uhakika, safi na usiotegemea mabwawa ya maji,” alisema Rais Hichilema.

Rais Hichilema aliipongeza Amsons Group akisema mradi huo wa nishati ya jua utaiwezesha Zambia kutimiza, na huenda kuzidi, lengo lake la kuongeza megawati 1,000 za nishati ya jua kwenye gridi ya taifa, hatua ambayo itahakikisha kukoma kwa mgawo wa umeme na kuweka mazingira thabiti ya ukuaji wa uchumi.

1
Nahdi alisema Amsons Group na wadau wake wanajivunia kushirikiana na Zambia katika mradi ambao unachochea mabadiliko ya kimkakati kwenye sekta ya nishati.

“Mradi huu hauhusu tu kuzalisha umeme, bali kujenga ajira endelevu, kuongeza uwezo wa ndani na kujenga mifumo imara ya nishati itakayohudumia makazi, shule na viwanda kwa miongo ijayo,” alisema Nahdi.

Uwekezaji wa Dola milioni 600 katika kituo cha umeme wa jua chenye uwezo wa Gigawati moja unatajwa kuwa moja ya miradi mikubwa zaidi ya uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI) katika sekta ya nishati Zambia na Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Mradi huo unatabiriwa kupunguza utegemezi mkubwa wa Zambia kwa umeme wa maji, hali iliyosababisha upungufu wa umeme kutokana na ukame unaochochewa na mabadiliko ya tabianchi.

Mkurugenzi wa Exergy Africa Limited, Monica Musonda, alisema ushirikiano huo unaonesha kuongezeka kwa kasi kwa juhudi za Kiafrika kuunganisha sekta ya nishati na kutatua pengo la miundombinu kwa kutumia ushirikiano wa biashara zenye mizizi barani Afrika.

Naye, Waziri wa Nishati nchini Zambia, Makozo Chikote, alisema serikali inaendelea kuvutia uwekezaji wa sekta binafsi kama ishara ya mkakati imara wa nishati unaohusisha ushindani na ubunifu baina ya sekta binafsi na ya umma.