KISIWA CHA UZI: Kina kituo cha afya chenye daktari na mkunga mmoja, wakazi 4,200

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 02:16 PM Nov 26 2024
Mwonekano wa jengo la Kituo cha Afya Uzi lililojengwa na serikali kupitia TASAF. Jengo hilo lilizinduliwa mwaka 2023 na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdalla.
Picha: Rahma Suleiman
Mwonekano wa jengo la Kituo cha Afya Uzi lililojengwa na serikali kupitia TASAF. Jengo hilo lilizinduliwa mwaka 2023 na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdalla.

KWA Zanzibar, serikali inajivunia kufikia lengo la kuwa na kituo cha kutolea huduma za afya kila baada ya umbali kilomita tano.

Hata hivyo, upatikanaji huduma za afya katika vituo hivyo ni si wa uhakika, mwandishi wa habari hizi anaripoti kinachojiri visiwani katika wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Katika Kisiwa cha Uzi wilayani humo, kuna shehia mbili zenye wakazi 4,233. Hizo ni Uzi yenye 3,075 (wanawake 1,510 na wanaume 1,565) na Ng’ambwa yenye wakazi 1,158 (wanawake 571 na wanaume 587). Wote wanategemea Kituo cha Afya Uzi kupata huduma za afya. 

Ni kituo kinachotoa huduma za matibabu muda saa za kazi tu; kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri siku za wiki (Jumatatu hadi Ijumaa). Wikiendi hakuna huduma inayotolewa kituoni huko.

Uzi ni miongoni mwa visiwa 52 vinavyoizunguka Zanzibar (saba vinakaliwa na watu vikiwa na huduma muhimu kama vile umeme, maji na vituo vya afya).

Kilio kikubwa cha wakazi wa kisiwani Uzi ni kukosekana watoa huduma za uzazi, jambo wanalolitaja linaweka hatarini uhai wa mama na mtoto.

Zahra Muhamed Muazini (26), mkazi wa kisiwa hicho, almanusura apoteze uhai baada ya kujifungua akiwa katika boti saa nane usiku wakati akipelekwa kupata huduma nje ya kisiwa hicho.

"Ninakumbuka ilikuwa Januari mwaka huu, saa nane usiku, uchungu umenikaza, kituo chetu cha afya hakifanyi kazi kwa muda huo lakini pia hakina daktari wa huduma ya mama kujifungua," anasimulia Zahra.

Mama huyo wa watoto wanne anaendelea: "Wakati uchungu umekaza, maji ya bahari nayo yameshafungamana kisiwani, huwezi kutumia mtumbwi wa kawaida kutoka nje ya kisiwa, lazima utumie usafiri wa boti.

"Usafiri unaotumika kisiwani hapa ni gari au bodaboda (pikipiki) kwa nyakati ambazo maji ya bahari hayajaingia kisiwani na kufunga barabara. Kutoka hapa Uzi hadi kijiji cha Unguja Ukuu ni wastani wa kilomita tatu.

"Gharama za usafiri wa boti ni Sh. 1,500 kwa kila abiria, lakini nyakati za dharura, mfano wa kumsafirisha mjamzito kwa boti ni Sh. 30,000 na ni mwendo wa dakika 10 unaotumika kutoka hapa Uzi hadi Unguja Ukuu kwa usafiri wa boti."

Zahra anasema kuwa wakiwa katikati ya bahari, akipelekwa Kituo cha Afya Unguja Ukuu, alijifungua chini ya usimamizi wa mkunga wa jadi aliyemsindikiza.

"Wakati ninatoka nyumbani kwangu, niliongozana na baadhi ya wanafamilia pamoja na mkunga wa jadi ambaye hutusaidia kutuzalisha wakati wa dharura hapa kisiwani.

"Ni jambo la kusikitisha kwamba, kisiwa cha Uzi kina kituo cha afya kizuri, chenye vifaa tiba, lakini hakina wataalamu wa huduma za uzazi.

"Hii kero inatukwaza na kutudhalilisha sisi wanawake kwa sababu wakati wa kujifungua kunahitaji faragha chini ya usimamizi wa wataalamu wa afya.

"Kwa kweli siku ile sitoisahau maishani mwangu, kujifungua katika boti! Lakini ninamshukuru Mungu alinisaidia nikajifungua salama mtoto wangu wa kike ambaye hivi sasa anakaribia kutimiza umri wa mwaka mmoja," anasema Zahra.

Rai yake kwa serikali ni kuwapatia wataalamu wa afya ya uzazi ili kinamama wajifungue katika Kituo cha Afya Uzi na kuokoa maisha ya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Mkasa wa Zahra unafanana na wa Ada Sheha (30), mama wa watoto sita na mkazi wa kisiwa hicho aliyejifungua ndani ya gari wakati akiwahishwa Hospitali ya Unguja Ukuu nje ya kisiwa hicho.

"Mwaka jana (2023), nikiwa na ujauzito wa mtoto wangu wa tano, nilijifungua ndani ya gari mchana kweupe baada ya kukosa wataalamu wa afya katika Kituo cha Afya Uzi.

"Wakazi wa kisiwa hiki wanapobeba ujauzito huwa na hofu kutokana na kituo kutokuwa na wataalamu wa uzazi, hivyo baadhi hulazimika kuyahama makazi yao wanapokaribia kujifungua kwa kwenda kuishi kwa ndugu na jamaa nje ya kisiwa hiki.

"Mimi mimba zangu zote nimejifungua kwa wakunga wa jadi hapa kisiwani. Hii mimba yangu ya mtoto wa tano nilitaka nijifungulie hospitalini kwa sababu wakunga wa jadi sasa wamekatazwa kuzalisha, lakini sikufika hospitalini, nikajifungua ndani ya gari. 

"Nilibahatika kuzaa mtoto wa kiume ambaye ni huyu hapa unayemwona," anasema mama huyo huku akimwonesha mwandishi mtoto wake wa tano na mwingine mchanga wa kike anayemtaja amejifungulia kwa mkunga wa jadi kisiwani huko miezi mitano iliyopita.

Ada anaungana na mwanamama mwenzake Zahra kupaza sauti dhidi ya ukosefu wa watoa huduma za uzazi kisiwani kwao, akiomba serikali ipeleke watumishi wa kutosha katika kituo hicho ili wananchi wasisumbuke.

Ramadhan Haidari (43), baba wa watoto watano katika kisiwa hicho, anasema kituo chao kina daktari mmoja, hivyo wanahitaji wataalamu wa afya wa kutosha na wawapo kituoni muda wote ili wake zao wasijifungulie kwa wakunga wa jadi.

"Tatizo hili haliwaumizi wanawake tu, hata sisi wanaume linatuumiza, tunapata tabu sana katika kupata huduma. Mimi binafsi nilikwenda na mke wangu katika kituo hicho ili apate huduma ya kujifungua lakini kutokana na kituo kutokuwa na wataalamu wa uzazi, nilimsafirisha kumpeleka Kituo cha Afya Unguja Ukuu, ile tunafika tu, akajifungua.

"Kama tungechelewa kidogo tu kumfikisha Kituo cha Afya Unguja Ukuu, angejifungulia njiani. Kama hatuna wataalamu wa afya, ninafikiri serikali iendelee kuwapa fursa wakunga wa jadi kuzalisha ili kuwasaidia wajawazito kisiwani kwetu," anasema Haidari.

MKUNGA WA JADI

Mtoro Ali Hassan (56), mkunga wa jadi kisiwani Uzi, anasema serikali imepiga marufuku wakunga wa jadi kuzalisha na badala yake wawaongoze wazazi kwenda kujifungua kituo cha afya.

Hata hivyo, kutokana na ukosefu wa watoa huduma za afya kisiwani Uzi, Mtoro anasema hulazimika kuwasaidia kinamama kujifungua hasa nyakati za dharura.

"Ni mimi niliyemdhalisha Zahra Muhamed Muazini tukiwa katika boti wakati akiwahishwa Kituo cha Afya Unguja Ukuu. Nililazimika kutoa msaada ili kuokoa uhai wake na mtoto, na siku hiyo ilikuwa ngumu kwangu maana sikuwa na zana yoyote," anasimulia mkunga wa jadi.

Mkunga wa jadi huyo anasema kisiwa hicho kimezungukwa na bahari, hivyo kinahitaji kuwa na huduma muhimu, zikiwamo za afya kwa saa zote 24 kwa siku zote za wiki. Wataalamu wa afya wawapo kisiwani muda wote.

"Uzazi hivi sasa ni mgumu, wakati mwingine anakuja mzazi nyakati za usiku anahitaji msaada, lakini hana zana yoyote ya kutumia kwa ajili ya kujikinga na maradhi, ninalazimika kutumia zana za kijadi, zikiwamo khanga ili kuwahudumia wanawake wenzangu," alisema mkunga huyo anayejitambulisha alianza kazi hiyo miaka 20 iliyopita.

Mkunga wa Jadi Mtoro anaomba Wizara ya Afya kuwashirikisha wakunga wa jadi ili kuwasaidia wananchi, hasa wanaoishi visiwani ambao wanakabiliwa na changamoto kupata usafiri wa baharini.

Anasema kuwa licha ya serikali kukataza wakunga wa jadi kuzalisha, baadhi ya wananchi wakaadi. Hukaa nyumbani mpaka uchungu unapokaza, hivyo kuwa vigumu kwao kukifikia kituo cha afya, hata kuangukia mikononi mwa wakunga wa jadi kupata msaada.

"Ninaungana na serikali kwamba uzazi wa sasa ni mgumu kulinganishwa na zamani kutokana na matatizo mbalimbali ya kiafya, hivyo ni sahihi kabisa wajawazito wakajifungulie hospitalini, lakini panapohitajika msaada wa dharura, tupo tayari kusaidia," anahitimisha Mtoro.

UONGOZI WA SHEHIA

Othman Mwinyi Haji, Sheha wa Shehia ya Uzi, anakiri kuwapo changamoto ya wataalamu wa afya katika Kituo cha Afya Uzi, akisema: "Kituo chetu cha afya ni kizuri mno, tumejengewa na serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF). Kina vifaa tiba vinavyohitajika na tena tuna mpaka nyumba za kuishi madakrati, lakini kituo hakitoi huduma kwa saa 24.

"Nyumba za madaktari zilizoko hawaishi na hao wachache waliopo katika kituo chetu cha afya wanakuja na kuondoka. Changamoto hii tumeshaiwasilisha katika ngazi za juu serikalini, wananchi kuendelea kuvumilia, serikali itatatua changamoto hii.

"Nyakati za usiku wananchi wa kisiwa hii, hasa wajawazito wanapata shida kutafuta huduma za afya na wakati mwingine hulazimika kujifungulia njiani kabla ya kufikishwa hospitalini au kujifungulia kwa wakunga wa jadi, jambo ambalo ni hatari kwa afya ya mama na mtoto."

WASIMAMIZI WA KITUO

Daktari Dhamana wa Kituo cha Afya Uzi, Seleh Nila Ali, anasema changamoto iliyopo ni uhaba wa wafanyakazi, hasa kwa wakunga. Kituo hicho kina mkunga mmoja na kutokana na uhaba wa wataalamu wa afya kinashindwa kuwazalisha wajawazito.

Anabainisha kuwa kwa mwezi kituo kinatoa huduma kwa wastani wa watu 500 wanaofika kupata huduma. 

Kati yao, watoto ni 100 na wajawazito 60 ambao hufuata huduma za awali, ikiwamo kuangalia maendeleo ya mtoto tumboni (kliniki).

Daktari huyo anasema kituo kina upungufu wa wakunga watano na madaktari watatu ili kukidhi mahitaji ya kutoa huduma za afya. Anaitaja kero hiyo ni kiini kinamama kisiwani huko kujifungulia kwa wakunga wa jadi.

"Rai yangu kwa wananchi wa kisiwa hiki ni kuhamasisha watoto wao kusoma masomo ya sayansi ili kupata wataalamu wa afya wazawa katika kisiwa hiki kwa sababu watu kutoka nje ya kisiwa hiki wanakuwa wagumu kuja kufanya kazi huku kutokana na changamoto ya usafiri," anasema.

Daktari Dhamana wa Wilaya ya Kati Unguja (DMO), Dk. Amina Hussein Pandu, anasema Kituo cha Afya Uzi kina hadhi ya daraja la kwanza, hivyo hakina uhaba mkubwa wa wataalamu wa afya na serikali inajitahidi kuongeza wataalamu kila inapohitajika. 

"Kutokana na jiografia ya kisiwa hicho, kinahitaji kuwa na boti za kubebea wagonjwa. Serikali itakapojitosheleza katika hili haitosita kutoa huduma za uzazi katika kituo hicho maana uzazi si jambo jepesi. 

"Raha ya mama anapokwenda kujifungua, arudi na mwanawe na uzazi una changamoto nyingi, lazima hivi vitu vyote vifanyiwe utaratibu ndipo shughuli za kuzalisha zitakapoanza kituoni," anasema Dk. Amina.

Anasema awali kisiwa cha Uzi hakikuwa na kituo kikubwa cha afya chenye vifaa vya kisasa na kwa sasa mama mjamzito ana uwezo wa kufanya vipimo, vikiwamo vya Utrasound, hivyo anawataka wananchi kuendelea kuwa wavumilivu wakati serikali inatatua changamoto zinazowakabili.

Kisera, Dk. Amina anasema kituo cha afya cha daraja la kwanza kinapaswa kutoa huduma kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 9:00 alasiri na kinapaswa kuwa watoa huduma wasiopungua 10.

Anasema Kituo cha Afya Uzi kina vifaa muhimu, vikiwamo vya dharura kwa ajili ya wajawazito kujifungulia, lakini kinakabiliwa na changamoto ya kutokuwa na watoa huduma.

Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdullah, anasema serikali imefanya mageuzi makubwa katika sekta ya afya kwa kuboresha huduma hizo na inaendelea kuwasomesha wafanyakazi ili kuwa na wataalamu bingwa watakaotoa huduma bora kwa wananchi mijini na vijijini.

Anasema serikali pia inaendelea kuweka mazingira bora ya utoaji huduma za afya na kwamba, kwa mwaka huu wa fedha (2024/25), watumishi wapya 1,566 wataajiriwa ili kuleta ufanisi zaidi katika utoaji huduma za afya kwa wananchi.