Saranga wajivunia kampeni uhamasishaji uchaguzi Serikali za Mtaa kuzaa matunda

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 07:15 PM Nov 26 2024
Mjumbe wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kata ya Saranga, Menidora Mpogole.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mjumbe wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kata ya Saranga, Menidora Mpogole.

WAKATI Watanzania Bara, wakijiandaa kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika kesho, suala la ushirikishwaji wa makundi yote na uwakilishi sawa limepewa kipaumbele.

Wagombea, vyama vya siasa, na mashirika ya kijamii wanasisitiza umuhimu wa kuondoa vikwazo vinavyowakabili wanawake na vijana kama hatua muhimu kuelekea demokrasia jumuishi.

Wadau wa kisiasa, viongozi wa vyama vya upinzani, na mashirika ya kijamii wamelitaka serikali kuunda mazingira yenye usawa wa fursa kwa kila mwananchi.

Makamu Mwenyekiti wa Kituo cha Maarifa na Taarifa Kata ya Saranga, jijini Dar es Salaam, Hancy Obote, anasema ni muhimu kwa vyama vya siasa kurekebisha kanuni zao ili kuondoa vikwazo vinavyowazuia makundi yaliyotengwa kushiriki kikamilifu.

Anasema kuwa miongoni mwa kanuni zinazohitaji marekebisho ni zile zinazoweka masharti ya kuwa mwanachama kwa zaidi ya miaka mitano kabla ya kugombea nafasi. Hii ni changamoto kwa wanawake na vijana wengi wana hamasa ya kisiasa lakini hawana uzoefu wa muda mrefu.

Aidha, vyama vinapaswa kupunguza ada kubwa za uanachama na za kugombea, kwani ada hizo ni mzigo kwa wanawake na vijana wengi, na huwazuia kushiriki katika uchaguzi.

Pia,kanuni zinazohusiana na uwiano wa kijinsia zinapaswa kurekebishwa ili kuhakikisha nafasi za uongozi zinapatikana kwa usawa kwa wagombea wa kiume na wa kike.

Kurekebisha vigezo vya elimu na uzoefu wa kisiasa ni muhimu ili wanawake na vijana wenye uwezo wa uongozi, lakini ambao hawafikii vigezo vya juu, waweze kushiriki kikamilifu.

Makamu Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kata ya Saranga, Hancy Obote akizungunza na Mwandishi wa Nipashe (huyupo pichani) kuhusu ushiriki wao kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Obote anasema mifumo ya uteuzi wa wagombea inapaswa kuzingatia usawa wa kijinsia na kutoa fursa sawa kwa wanawake na vijana katika mchakato wa uchaguzi.

 "Ushirikishwaji wa wanawake na vijana si tu unaimarisha demokrasia, bali pia unawezesha matumizi bora ya uwezo wao katika uongozi na maendeleo ya jamii," anasema Obote.

Kituo hicho kimeendesha kampeni za uhamasishaji kwa lengo la kuwahimiza wanawake na vijana kushiriki katika mchakato wa uchaguzi, na juhudi hizo zimezaa matunda.

"Tunaona idadi kubwa ya wanawake wamejitokeza kugombea nafasi mbalimbali, hatua inayodhihirisha mafanikio ya juhudi zetu," anaongeza.

Hata hivyo, changamoto kadhaa zimejitokeza, ikiwa ni pamoja na umbali wa vituo vya kupigia kura, miundombinu duni, na masharti magumu ya vyama vya siasa yanayowazuia baadhi ya wananchi kugombea nafasi za uongozi.

Obote anazungumzia changamoto za miundombinu  hususani barabara kuwa zinakwamisha mchakato wa uchaguzi, anasema ukubwa wa kata yao ungeweza kugawanywa kuwa kata tatu ili kurahisisha usafiri wa wananchi kwenda kwenye vituo vya kupigia kura.

Anaeleza kuwa milima iliyopo katika maeneo hayo inafanya usafiri kwa pikipiki, baiskeli, au magari kuwa mgumu, na hivyo wananchi wengi wanalazimika kutembea umbali mrefu kufika kwenye vituo vya kupiga kura.

Makamu Mwenyekiti wa Kituo cha Taarifa na Maarifa Kata ya Saranga, Hancy Obote akizungunza na Mwandishi wa Nipashe (huyupo pichani) kuhusu ushiriki wao kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
"Obote anasema ameiona changamoto hiyo baada ya kujisajili katika eneo hilo ili kufahamu umbali wa vituo vya kupigia kura.

'Nilitembea kwa dakika 45 chini ya jua kali, na kumbuka nilitembea kwa miguu, sasa fikiria mwanamke mwenye mtoto mgongoni au mjamzito, katika maeneo ambapo vituo vya usajili viko mbali, bado wanapata changamoto kubwa kufika kwenye vituo vya kupiga kura kutokana na hali ngumu ya kijiografia.'"

Mwakilishi wa Kata ya Saranga kupitia  Chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema, Menidora Mpogole, anasema wanashukuru  wagombea walioenguliwa kurejeshwa kwenye mchakato wa uchaguzi.

"Tumeona kamati ya kisiasa imechukua hatua. Katika mitaa yetu, wale waliokuwa wameenguliwa sasa wamerejeshwa,hii inaashiria kwamba wale waliokuwa wameenguliwa sasa watapiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa," anasema.

Katika hotuba yake ya hivi karibuni, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan aliwahimiza Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchaguzi huu, akisisitiza umuhimu wake kama sehemu ya kujenga msingi wa demokrasia ya uwakilishi.

"Ni fursa muhimu kwa wananchi wote kushiriki katika kuimarisha uongozi wa mitaa, hatua inayochochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi," anasema Rais Samia.

Anasema kwa kuzingatia umuhimu wa uchaguzi huu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeahidi kusimamia mchakato kwa uwazi na ufanisi, huku wananchi wakihimizwa kushiriki kupiga kura.