Lissu asema hana mrithi nafasi yake CHADEMA

By Restuta James , Nipashe
Published at 08:42 AM Dec 14 2024
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ametangaza kuwa hana mgombea wa kurithi nafasi yake ndani ya chama hicho.

Amesema yuko tayari kufanya kazi na yeyote ikiwa yeye atachaguliwa kuwa mwenyekiti.

Wakati Lissu anasema hayo, Kamati Kuu ya CHADEMA imetangaza leo kukutana Dar es Salaam, huku agenda zake zikiwa ni pamoja na usaili na uteuzi wa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi Kanda za Kaskazini na Kati na maandalizi ya Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa chama ngazi ya taifa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii jana,  Lissu alisema atafanya kazi na Makamu Mwenyekiti yeyote atakayechaguliwa na kuwataka wajumbe wamchague mtu mwadilifu.

Kauli hiyo ameitoa ikiwa ni siku moja baada ya kutangaza kugombea uenyekiti wa taifa wa CHADEMA ambayo kwa sasa inashikiliwa na Freeman Mbowe. 

“Yeyote ambaye atajitokeza na hana mawaa, mimi nitakwenda naye, hatuhitaji watu wenye mawaa, lakini sio mimi nitakayechagua Makamu Mwenyekiti, itabidi ajitokeze. Akichaguliwa mwenye mawaa itakuwa shida,” alisema Lissu.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Itifaki na Mambo ya Nje ya chama hicho, John Mrema, kwa vyombo vya habari,  ilisema kikao hicho kitaongozwa na Mwenyekiti Mbowe.

Wakati Kamati Kuu ikijifungia, taarifa za ndani ya chama hicho zinasema  uchaguzi wa viongozi wa taifa CHADEMA utafanyika mwezi ujao.

Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, alisema mwezi na tarehe ya uchaguzi itatangazwa Jumatatu ijayo.

Kuhusu idadi ya makada ambao wamejitokeza kuwania uenyekiti na makamu mwenyekiti, Mnyika alisema wote wanaojitokeza anawasilisha majina kwenye Kamati Kuu, ambayo inatoa ruhusa ya kuyatangaza au kutotangaza.

“Kwa wale ambao wameshajitangaza, ninaweza kuthibitisha kwamba, nimepokea barua zao. Nimepokea ya (barua ya) Mheshimiwa Lissu,” alisema.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa baadhi ya makada ambao wameonesha nia ya kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti ni Hezekiah Wenje, ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Kanda ya Ziwa Victoria. Wenje pia aliwahi kuwa mbunge wa Nyamagana, jijini Mwanza.

Wengine wanaotajwa ni John Heche ambaye pia amewahi kuwa Mbunge wa Tarime na Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema.

Hata hivyo, Nipashe ilipomtaka Lema ili kujua ikiwa atagombea nafasi hiyo, alisema kwa sasa amejiweka kando na siasa.

“Kwanza mimi sipo Tanzania, nipo Canada. Siasa nitafanya kwa kiasi kidogo sana, nimeamua nipumzike kidogo,” alisema.

Wakati Lissu akitoa msimamo huo, makada wa CHADEMA wameendelea kunyukana mitandaoni.

Miongoni mwa makada wanaonyukana ni Meya wa zamani wa Ubungo ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Kanda ya Pwani, Boniface Jacob, Martin Masese, aliyekuwa mgombea wa CHADEMA Mbarali, Liberatus Mwang’ombe, Yeriko Nyerere na makada wengine.

Kwa upande wake, Mwanaharakati Maria Sarungi, ametangaza kumuunga mkono Lissu, akieleza kuwa ni kiongozi makini anayetosha kukiongoza chama hicho katika kipindi hiki.

Juzi, Lissu alitangaza kumkabili Mbowe kwenye nafasi ya Uenyekiti wa CHADEMA, akiwa na agenda saba, ikiwamo ya kuisuka upya Katiba ya chama hicho, ili pamoja na mambo mengine kuweka ukomo wa uongozi wa chama, ubunge na udiwani wa viti maalum na kutengeneza mifumo ya kusimamia chaguzi huru na za haki.