MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ametangaza kumvaa Freeman Mbowe, kugombea Uenyekiti wa chama hicho hicho.
Lissu ametangaza kuwania uenyekiti katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Desemba 12, 2024, uliohudhuriwa pia na makada wa chama hicho kutoka kanda zake nane, wakiwa wamebeba mabango.
mabango yaliyobebwa na makada hao yameandikwa 'Tundu Lissu ni yeye 2024/29 haki huinua taifa.'
Amesema ameamua kugombea ili kuweka mbinu za kufanya siasa katika mazingira ya sasa, ikiwamo kuisuka upya Katiba ya CHADEMA na kuweka ukomo wa uongozi katika ngazi mbalimbali ndani ya chama hicho.
Amesema ukomo wa uongozi utawekwa pia kwa wabunge wa Viti Maalum na Madiwani.
Amesema CHADEMA kimejengwa katika msingi mzuri na waasisi wake, akitolea mfano kwamba Mzee Edwin Mtei na Bob Makani, ambao walikaa madarakani kwa awamu moja pekee na kuandaa warithi wao.
"Wazee wetu hawa walikuwa wasomi waliosomeshwa katika mila na desturi za kisiasa za Kiingereza. Bila shaka walikuwa wanafahamu, na walizingatia, funzo la kutong’ang’ania madaraka lililotolewa na Oliver Cromwell, kwa wabunge wa Uingereza mwaka 1653 wakati wa vita kati ya wafuasi wa Bunge na wa Mfalme Charles I," amesema.
Amesema Cromwell aliwaambia wabunge hao kuwa: "Mmekaa hapa kwa muda mrefu sana kwa mazuri yoyote ambayo mmekuwa mkiyafanya. Ondokeni, nasema, ili tumalizane nanyi. Kwa jina la Mungu, nendeni zenu.”
Amesema anaamini kuwa Mtei na Makani, walifahamu historia hiyo na ndio sababu hawakutaka kukaa madarakani mpaka watakapolazimishwa kuondoka.
Amesema waliandaa utaratibu wa kuondoka madarakani kwa hiari yao na kwa kutumia taratibu za kikatiba.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED