Manispaa kujenga vituo vya afya kila kata

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 01:33 PM Jun 28 2024
Mweka hazina wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga,Gordon Dinda akiwasilisha taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa serikali(CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/2023 wakati wa kikao maalumu cha baraza la madiwani cha kujibu hoja za CAG.
PICHA: SHABAN NJIA.
Mweka hazina wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga,Gordon Dinda akiwasilisha taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa serikali(CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/2023 wakati wa kikao maalumu cha baraza la madiwani cha kujibu hoja za CAG.

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, imesema itaendelea kutenga fedha kila kwa ajili ya kujenga vituo vya afya kila kata ili kusogeza huduma karibu na wananchi na kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za matibabu ikiwemo ya uzazi.

Pia watajenga zahanati kila kijiji katika vijiji 44 kwani kwa sasa ni vijiji 18 vilivyo na zahanati na vijiji 26 vilivyobaki vitasogezewa huduma hiyo kila mwaka wa fedha na kuhakikisha vinakuwa na vifaa tiba pamoja na madawa ili kuondoa malalamiko ya kukamilisha ujenzi na kutokutoa huduma kwa wakati.

Hayo yamebainishwa na Mweka Hazina wa Manispaa hiyo,Gordon Dinda wakati akiwasilisha taarifa ya Makaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali(CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/2023 na kupata hati safi kwa kujibu hoja 25 zilizotakiwa kujibiwa.

Amesema, kila mwaka wa fedha watahakikisha wanajenga kituo cha afya ili kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia fedha za mapato ya ndani, kati ya kata 20 zilizopo ni kata nne tu zenye vituo vya afya na kata 16 hazina huduma hiyo,na itasaidia kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi kwa wajawazito.

Diwani wa halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wakifuatilia taarifa ya CAG inayotolewa na Mwaka hazina Gordon Dinda.PICHA: SHABAN NJIA.
"Vituo hivi vinne vilivyopo vipo umbali wa kilometa 15 hivyo inalazimika kutumia gari la kubeba wagonjwa kutoka kituo cha afya Mwendakulima, na havina huduma ya kuhifadhi maiti na macho isipokuwa huduma nyingine zinapatikana na tutahakikisha huduma hizi zinapatikana" amesema  Dinda.

Aidha amesema, sera ya serikali za mitaa inawaelekeza kununua dawa moja kwa moja katika bohari ya dawa ya Taifa(MSD) hivyo wataendelea kununua dawa na kuzifikisha katika vituo vya afya na zahanati ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa dawa kwa wanaofika vituoni kupata huduma.
Wajumbe mbalimbali wakifuatilia kikao Cha CAG katika Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama; PICHA: SHABAN NJIA.
Hata hivyo Manispaa ya Kahama imeendelea kupata hati safi miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka wa fedha 2020/2021, 2021/2022 pamoja na mwaka wa fedha 2022/2023 na nikwasababu ya kuendelea kujibu hoja ipasavyo pasipo kuacha shaka ya aina yoyote.

Wajumbe mbalimbali wakifuatilia kikao Cha CAG katika Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama; PICHA: SHABAN NJIA.