NEMC yatoa tahadhari ya mvua kubwa,maporomoko ya ardhi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:25 AM Feb 02 2025
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Semesi.
Picha:Mtandao
Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Semesi.

Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetoa onyo la dharura kwa wananchi kuhusu hatari inayoweza kusababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha, pamoja na maporomoko ya ardhi yanayoweza kuleta madhara makubwa kwa maisha na mali.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Immaculate Semesi, akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, amesisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ambazo zimeendelea kuwa tishio kubwa kwa mazingira na jamii.

Dk. Semesi ameainisha madhara yaliyosababishwa na maafa yaliyopita, yakiwemo maporomoko ya ardhi yaliyotokea Katesh (Manyara), Kawetere (Mbeya), na Mamba Miamba (Kilimanjaro), pamoja na mafuriko makubwa yaliyokumba maeneo ya Rufiji, Morogoro, na Kilombero. Maafa haya yamesababisha vifo vya watu, uharibifu wa mali, na kuathiri miundombinu muhimu kama barabara, madaraja, na mtandao wa umeme.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetabiri mvua zitakazozidi wastani katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mara, Arusha, Kilimanjaro, na Manyara, huku maeneo mengine yakitarajiwa kupokea mvua kubwa. Dk. Semesi ameonya kuwa hali hii inaweza kusababisha mafuriko makubwa, maporomoko ya ardhi, na uharibifu wa makazi, mashamba, na miundombinu muhimu.

Kutokana na hali hii, NEMC inatoa wito kwa wananchi kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mamlaka husika, ikiwa ni pamoja na kuhama maeneo hatarishi, kuchukua hatua za kuzuia uharibifu wa mazingira, na kushirikiana na serikali katika juhudi za kupunguza athari za maafa yanayoweza kutokea.