Simba, Tabora Utd mwisho wa tambo

By Somoe Ng'itu ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:24 AM Feb 02 2025
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids
Picha: SSC
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids

KUCHEZA kimkakati ili kupata ushindi ndio jambo muhimu kwa Simba kuelekea mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Tabora United itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani, Tabora.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, alisema jana wamejipanga kuikabili Tabora United 'kimkakati', kwa sababu wanafahamu ni timu nzuri na iliyoimarika zaidi kwa sasa.

Fadlu alisema wamejiandaa kucheza kwenye uwanja ambao ana wasiwasi  hautafanya wawe na uhuru wa kumiliki vyema mpira kwa kiasi kikubwa.

Kocha huyo alisema kikosi chake kipo tayari kukabiliana na kila aina ya ushindani katika mchezo huo kwa sababu wako imara kwa ajili ya mashindano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika pamoja na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ujumla na si kwa ajili ya Tabora United pekee.

 "Kwanza kabisa tulikuwa tunajiandaa kwa ajili ya mechi za Kombe la Shirikisho na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na wala siyo kwa ajili ya Tabora United, lakini pamoja na hayo tunaiheshimu sana, ina wachezaji wazuri, ila tutakwenda kucheza kama tunacheza na timu nyingine, lakini uwanja nao unaweza kutuamulia mfumo ambao tutatakiwa kucheza, najua hauwezi kutupa uhuru sana kama inavyokuwa Benjamin Mkapa au KMC Complex," alisema Fadlu.

Aliongeza kutokana na hilo mechi hiyo itachezwa kimkakati zaidi, huku akiwa ameshajua maeneo hatari ya wapinzani wao yanapotokea.

Kocha Mkuu wa Tabora United, Anicet Kiazayidi, alisema tayari maandalizi ya mchezo huo yamekamilika na wachezaji wake wapo fiti, anachosubiri ni dakika 90.

"Maandalizi yamekamilika,  wachezaji wako fiti japo ratiba ilibana kidogo kwa kurejeshwa nyuma Ligi Kuu, ila nimeiandaa timu vizuri ili kwenda kupambania ushindi," alisema Mkongomani huyo.

Ligi Kuu Tanzania Bara itaendelea tena Jumatano kwa Tabora United kuivaa Namungo wakati KenGold itawafuata mabingwa watetezi, Yanga na Dodoma Jiji itawaalika Pamba Jiji kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini, Dodoma.