KATIKA kuhakikisha haitaki kupigana vikumbo kugombea wachezaji baada ya msimu kumalizika, Azam FC imeanza mchakato wa usajili mapema na tayari imetangaza kumnasa beki, Yoro Mamadou Diaby, kutoka Mali, ambaye pia ni mahiri katika ufungaji mabao.
Taarifa imetolewa na Azam imesema imemsajili mchezaji huyo kutoka katika Akademi ya Yeleen Olympique na ataanza kuonekana rasmi katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Azam imesema mchezaji huyo anayecheza beki wa kati alikuwa wakiichezea Stade Malien de Bamako kwa mkopo.
"Yoro amezichezea timu zote za vijana za taifa za Mali, kuanzia ile ya U-17, U-20 na U-23, na atajiunga rasmi na Azam FC kuanzia msimu ujao wa 2024/2025," imeandika taarifa hiyo.
Akiwa Stade Malien, ameisadia timu hiyo kufika robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, akifunga mabao katika mechi zote mbili za hatu hiyo dhidi ya Dreams FC ya Ghana, ingawa timu yake iliondolewa kwa jumla ya mabao 3-2.
Rekodi zinaonyesha katika mechi ya kwanza ya robo fainali, ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Machi 26, mwaka huu alifunga bao na matokeo yakimalizika kwa Stade Malien kuchapwa mabao 2-1 na mechi ya marudiano iliyochezwa kwenye Uwanja wa Baba Yara, Ghana Aprili 7, mwaka huu, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, Yoro akifunga tena bao dakika ya 59, kabla ya Sylvester Simba kusawazisha dakika ya 90.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED