Askofu wa Jimbo Katoliki Kahama, Mhashamu Christopher Ndizeye amewashauri waumini kuchangamkia fursa za mafundisho ya dini wanapotangaziwa kushiriki kwenye makongamano yenye mafundisho, mikutano, na nafasi za ibada ili kujua mafundisho sahihi ya imani zao, kutumia imani hiyo katika maisha yao ya kila siku kutatua changamoto zinazowakabili katika familia na Taifa kwa ujumla .
Mhashamu Christopher Ndizeye, Askofu wa Jimbo la Kahama alisema hayo leo katika Adhimisho la Misa Takatifu ya kutoa Sakramenti ya Kipaimara katika Parokia ya Mtakatifu Stephano Shahidi Nyasubi Kahama.
"Tupende kujua imani yetu, tupende kujua kanisa linatufundisha nini, na sisi kama kanisa tunapenda kuongeza vipindi shuleni lengo kuu ni kusaidia wanafunzi wajue nini kanisa linataka wajue," alisema.
Mbali na hilo, alishauri waumini watafute nafasi za kujua ukweli kuhusu imani yao, mafundisho sahihi ya imani yao na kuweka katika maisha Yao ya kila siku, kama Mtakatifu Stephano alivyojua imani yake na hatimaye akakubali kufa kwa sababu alijua huu Ndiyo ukweli kuhusu imani yake.
Alisema kanisa limekuwa likiandaa mikutano, kongamano na ibada mbalimbali zinazotoa mafundisho ya kiimani, lakini watu wanakuwa wazito kuhudhuria, waumini jitahidi kutafuta nafasi ya kujua mafundisho sahihi ya imani.
Lakini Pia ukijua mafundisho ya imani haitoshi, najua waumini mnajua sala nyingi sana kuanzia sara ya asubuhi hadi sara za jioni, lakini lazima twende hatua mbele, tunatumiaje imani yetu na sala tunazozijua katika maisha ya mwanadamu, katika maisha yetu ya kila siku? tunaitumiaje imani yetu kuleta amani katika familia zetu, kutatua changamoto tulizonazo katika familia zetu, kutoa haki na masuala mengine? Alihoji Askofu Ndizeye.
"Tunapozungumzia Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, tunaalikwa kula chakula cha kiroho kila siku, lakini kabla ya kula tunatakiwa kujichunguza, kuwa wasafi , lazima uungame usije kupokea hukumu yake," alisema Aliomba watoto waliopata Sakramenti ya Kipaimara kujua amri za Mungu, wachukue walichofundishwa wakiweke kwenye maisha yao ya kila siku.
Alisema katika ulimwengu tuliyonao sasa hivi, ukiona unasifiwa sana ujue unachukiwa, mimi natamani tuchukiwe, kama kuna kinyume na misingi ya Kanisa Katoliki, tusimamie ukweli. "Tuishi maisha halisi, siyo maisha ya kufikilika, hivi hofu tulizonazo watanzania, hivi kweli hakuna wakatoliki wanaosababisha hofu hizi? tuombe Mwenyezi Mungu atusaidie katika changamoto hii ili watanzania waweze kuishi kwa amani, wasiwe na hofu.
Aliwambia waumini kuwa, kama hawathamini Ekaristi Takatifu hakuna kitu,kwa sababu yote tunayoishi na kuyatenda yanatokana na Ekaristi Takatifu. Aliomba wakatoliki waliopo katika mazingira ya ngazi za serikalini, wawe wa shauri wazuri, wasikubali kila agizo linalotolewa, kama mamlaka hazikufundishi kutenda haki usifuate.
Lakini Pia kama Kuna changamoto zozote katika familia zetu, katika nchi yetu tukubali kushuka, tujadiliane, tuone tuna matatizo gani, tusimamie maadili ya dini yetu, lazima ukweli na haki visimame, tukubaliane kama hiki ni kibaya tukiache, kama ni kizuri tukifanyie kazi, watu wengi wana hofu.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED