Waziri aelekeza kufutwa tozo za Mahakama

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 09:50 AM Jan 02 2026
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe
PICHA: GRACE GURISHA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Riziki Shemdoe amemwelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuangalia uwezekano wa kufuta tozo za kiutawala za halmashauri zinazotakiwa kulipwa na Mahakama ya Tanzania wakati wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi nchini.

Profesa Shemdoe ametoa maelekezo hayo alipokuwa mgeni rasmi kwenye hafla ya kukabidhi eneo itakapojengwa Mahakama mpya ya Wilaya Lushoto kwa gharama ya fedha za ndani Sh. Bilioni 4.272.

Hatua hiyo imefikiwa kufuatia maombi manne yaliyowasilishwa na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel, kwa niaba ya Mahakama, ikiwemo ulipaji wa gharama za kiutawala wa kihalmashauri, pale panapohitajika viwanja vya ujenzi wa majengo ya Mahakama.

Mtendaji Mkuu alimweleza Waziri kuwa huduma zitakazotolewa na Mahakama baada ya kutekeleza miradi ya ujenzi huo itawanufaisha wananchi wa halmashauri husika. ‘Tunakuomba Waziri, kama ikikupendeza, kusamehewa hizi gharama za kiutawala ili kazi nyingine ziweze kuendelea,’ alisema.

Ombi lingine linahusu utoaji wa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama na nyumba za makazi kwa majaji na mahakimu, Profesa Ole Gabriel ameomba Wakuu wa Mikoa kuendelea kuratibu maelekezo ya Rais kuhusu TAMISEMI kushirikiana na Mahakama ya Tanzania na Wizara ya Fedha kuhakikisha Kata na Wilaya zote nchini zinapata majengo yake.

"Haya maelekezo aliyatoa Aprili 5, 2025 akiwa anazindua jengo la Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania jijini Dodoma. Naomba nikupe taarifa kwamba kuna pa kuanzia, wapo Wakuu wa Mikoa watatu, Rukwa, Katavi na Tanga, ambao tayari wameshalibeba suala hilo,’ alisema

Ombi lingine linahusu Wakuu wa Mikoa kutenga fedha kwa ajili ya kuwezesha kufanyika kwa Kamati za Maadili za Mahakimu, pia alimueleza kuwa wakuu wa Mikoa na Wilaya ni Wenyeviti wa Kamati hizo katika ngazi husika.

Ombi la nne linahusu ujenzi wa barabara itakayowezesha wananchi kufika kwa urahisi kwenye Mahakama hiyo mpya, pia alimuomba Waziri kuwaelekeza TARURA kutengeneza barabara angalau kwa changalawe kwa kuanzia kabla ya kiwango cha lami ili kumwezesha Mkandarasi kuendelea na ujenzi.

Akijibu maombi hayo kwa kuanzia na suala la gharama za utawala, Profesa Shemdoe  alisema, ‘Nadhani milioni 250 siyo fedha nyingi kihivyo, zinaweza kuondolewa na mambo mengine haya ya Mahakama yakaendelea,’ alisema 

Akizungumzia suala la Kamati za Maadili, Prof. Shemdoe pia amemwelekeza Katibu Mkuu kutoa mwongozo kwa mamlaka za Serikali za Mitaa ili kutenga bajeti kuwawezesha Wakuu wa Mikoa na Wilaya kusimamia Kamati hizo kwa ajili ya watendaji wa Mahakama.

“Hili ni jambo la msingi ambalo lipo kisheria na lipo kwenye utaratibu wa kazi za Viongozi hawa. Naomba utoke waraka wa kuweza kuwaelekeza Wakurugenzi kutenga bajeti kwenye eneo hili,” alisema.

Kuhusu kuwepo kwa majengo ya Mahakama kwenye kila Kata na Wilaya, Waziri Shemdoe alisema kuwa Desemba 16, 2025 alisaini barua kwenda kwa Wakuu wa Mikoa kuhakikisha wanalichukulia zoezi hilo kwa uzito mkubwa.

Pia, alisema amefurahi kusikia kuwa Wakuu wa Mikoa ya Rukwa, Katavi na Tanga wamekuwa mstari wa mbele, hivyo kwa mara nyingine aliwaelekeza Wakuu wa Mikoa 23 iliyobaki kulifanyia kazi jambo hilo na kulichukulia uzito unaostahili. 

Kuhusu TARURA, Waziri Shemdoe ameielekeza taasisi hiyo kuanzia Wilaya ya Lushoto, Mkoa wa Tanga na Makao Makuu kuhakikisha kwenye bajeti inayofuata wanatenga fedha kwa ajili ya barabara ya kwenda kwenye jengo hilo.