DC Nkinda awaagiza madiwani kusimamia miradi

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 04:42 PM Dec 29 2025
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda
Picha: Shaban Njia
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, amewataka Madiwani wa Manispaa ya Kahama kutumia nafasi zao za uongozi kuacha alama za kudumu katika maeneo yao kwa kusimamia kikamilifu na kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati.

Nkinda ameyabainisha haya leo wakati wa ufunguzi wa semina elekezi kwa madiwani wa Manispaa ya Kahama, mafunzo yanayotolewa na maafisa kutoka Chuo cha Serikali za Mitaa (Hombolo) cha jijini Dodoma. 

Semina hiyo imelenga kuwajengea uwezo madiwani kuhusu majukumu yao ya kisheria, uongozi bora, usimamizi wa miradi ya maendeleo na uwajibikaji kwa wananchi waliowachagua.

Amesema, madiwani wana jukumu kubwa la kusimamia rasilimali za umma na kuhakikisha fedha zinazotengwa, kwa ajili ya miradi mbalimbali zinatumika ipasavyo kwa manufaa ya wananchi.

Amedai uongozi unaopimika ni ule unaoacha matokeo chanya yanayoonekana katika maisha ya watu nasio kulala wakati unatambua wazi wananchi wanawahitaji.

“Madiwani mna dhamana kubwa kwa jamii, Wananchi wanawategemea kuona mabadiliko halisi katika kusimamia yale mliyoyaahidi katika uchaguzi. Hakikisheni mnasimamia miradi yote ya maendeleo kuanzia hatua ya mipango hadi utekelezaji wake," amesema Nkinda.

Aidha amewahizi pia kushirikiana kwa karibu na wataalamu wa halmashauri pamoja na viongozi wa mitaa na vijiji ili kutatua changamoto zinazowakabili wananchi kwa wakati, nakuongeza uwazi, uwajibikaji na mawasiliano mazuri na wananchi ni msingi muhimu wa uongozi bora.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Masudi Kibetu amesema, mafunzo hayo yatawasaidia madiwani kutoingiliana wakati wa utekelezaji wa majukumu kwani wengi wao ni wapya ukilinganisha na baraza la madiwani lililopita na watashirikiana kuongeza mapato ya ndani kwani fedha zinazopatokana zinarudi kwa wananchi kupitia miradi ya maendeleo.

Ofisa Tawala Mwandamizi-TAMISEMI, Mashaka Makuka amesema,mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha madiwani kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utawala wa serikali za mitaa. 

Ametaja mafunzo yatakayotolewa kuwa ni pamoja na Uongozi na utawala bora, Sheria za uendeshaji wa shughuli za serikali za mitaa, uendeshaji wa vikao, Mipango, Bajeti na usimamizi wa miradi ya Maendeleo, udhibiti wa fedha katika Mamlaka za Serikali za mitaa, usimamizi wa watumishi pamoja na ardhi.