Polisi Moro yaimarisha doria, yakamata watuhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo kupatikana na silaha, ulevi, meno ya tembo

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 10:31 AM Dec 26 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama
PICHA: IDA MUSHI
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama

JESHI la Polisi Mkoa wa Morogoro limeendelea kuimarisha operesheni zake dhidi ya vitendo vya uhalifu ambapo limewakamata watuhumiwa waliokutwa wa meno ya tembo, kumiliki silaha kinyume cha sheria na biashara haramu ya nyama ya pori.

Polisi wamemkamata Hussein Rashid (40), mkazi wa Ifakara, akiwa na silaha ya kienyeji aina ya Gobore na risasi 7 bila kibali pamoja na vipande 20 vya nyama ya pori aina ya Tohe huko katika eneo la Katinduka, Wilaya ya Kilombero. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP Alex Mkama amethibitisha hayo katika taarifa yake ya maandishi kwenda kwa vyombo vya habari ikizungumzia operesheni mbalimbali walizofanya. Aidha, Polisi waliendelea na ufuatiliaji na kufanikiwa kubaini watuhumiwa waliokuwa na silaha nyingine aina ya Gobore katika eneo la Chamwino, Manispaa ya Morogoro.

Katika operesheni hiyo hiyo, Jeshi la Polisi pia limefanikiwa kukamata watuhumiwa waliokuwa wakijihusisha na ujangili na kukutwa na meno ya tembo, hatua iliyotajwa kuwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya uhalifu wa wanyamapori nchini. Kamanda Mkama  ametoa shukrani kwa ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi na kuwataka kuendelea kutoa taarifa kwa ajili ya kudumisha amani na usalama wa taifa.