RAIS Samia Suluhu Hassan, amewakumbuka watoto 190 wenye ulemavu na wasio na ulemavu, wanaolelewa katika Shirika la The Creator Share Foundation lililopo Kata ya Kirua, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, baada ya kuwapa zawadi za sikukuu ya mwaka mpya.
Akizungumza leo Desemba 31,2025, alipokwenda kumwakilisha Rais Samia katika makabidhiano ya zawadi hizo, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu na Watu wenye ulemavu, Ummy Nderiananga, amesema ndani ya siku 100 za uongozi wake, ameendelea kuleta faraja, upendo, tumaini na umoja kwa Watanzania.
Amesema kuwa kitendo hicho, ni ishara ya upendo mkubwa kwa wananchi bila kujali hali zao. Kwa mujibu wa Naibu Waziri Ummy, Rais Samia ametoa wito kwa jamii kuwapenda, kuwajali na kuwahudumia makundi ya wenye mahitaji maalum, ili kukuza umoja na mshikamano katika Jamii.
"Mheshimiwa Dk. Samia katika utekelezaji wa utaratibu wake wa utoaji zawadi za sikukuu mbalimbali, msimu huu ni kuelekea sikukuu ya mwaka mpya wa 2026, amepeleka zawadi kwa watoto 190, wenye ulemavu na wasio na ulemavu wanaolelewa katika Shirika la The Creator Share Foundation.
Naomba nitumie fursa hii kuwatakia kheri ya sikukuu ya mwaka mpya wa 2026, twende tukasherehekee kwa amani na tukiwa na faraja. Kwa sababu, mheshimiwa rais ametukumbuka sisi watoto, hivyo niwaambie anatupenda sana hivyo tudumishe upendo huu miongoni mwetu kila mmoja amuone mwenzake ni wa muhimu katika jamii."
Amevitaja vitu alivyovikabidhi kwa watoto hao, ni pamoja na mchele kilo 100, ngano kilo 50, mbuzi wawili, sabuni, mafuta ya kupikia, madaftari, sukari kilo 25 na vinywaji.
" Nitoe wito kwa jamii kuwa, kila mmoja ana wajibu wa kuwahudumia watoto na watu wenye mahitaji maalum, siyo tu kwa siku za sikukuu, bali ni kwa muda wote ili kuwapa faraja na huo ndio upendo tunaotakiwa kuwaonesha," amesema Waziri Ummy.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, alisema ili kuwa na ustawi wa maisha ya kijamii, ni lazima kuwajali watu wenye uhitaji ili waweze kukidhi mahitaji muhimu ya kila siku.
Wakati, Diwani wa Viti Maalum, Pamela Chuwa, amepongea hatua hiyo ya Rais, Samia ya kuwafikia watu wenye ulemavu, akisisitiza jambo hilo linawafanya kujisikia nao ni sehemu ya jamii.
“Mimi kama mama mwenye mtoto wa mahitaji maalum nimejisikia furaha kwa kupewa kipaumbele na tumefurahi sana, Naibu Waziri Ummy, kutufikia ukizingatia baadhi yetu tumefukuzwa katika familia tukionekana kama kuzaa watoto wenye ulemavu ni mkosi na laana katika familia,” alisema Diwani huyo.
Vilevile, Ofisa Rasilimali Watu katika Shirika hilo, Judith Shio, baada ya kupokea zawadi hizo, amemshukuru Rais Samia, kwa moyo wa upendo na kuwajali watu wenye mahitaji maalum huku akitoa wito kwa wadau mbalimbali kujitolea ili kuendelezwa moyo wa upendo na faraja kwa makundi hayo.
“Kwa niaba ya Shirika, tunatanguliza shukrani zetu za dhati kwa upendo huu na mwaka huu tunauanza kipekee sana na watoto wamefurahi hivyo kwetu imekuwa faraja kubwa na imegusa jamii,”amesema Judith.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED