Samia aagiza mabadiliko jeshi la polisi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:03 PM Dec 26 2025
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan
PICHA: MTANDAO
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene ameweka wazi maelekezo aliyoagizwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ambayo yanaenda kugusa jeshi la polisi nchini.

Mabadiliko makubwa yakidhamiriwa ili kuboresha utendaji kazi wa jeshi hilo na kuweza kurejesha mahusiano mazuri na wananchi huku akiweka  wazi mabadiliko hayo kuwa ni kulibadili jeshi la polisi kutoka matumizi ya nguvu na kuwa jeshi la kutoa huduma na urekebishaji wa sheria katika suala la ukamataji wa watuhumiwa wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali.

Amesema hayo wakati wa mahojiano maalumu na waandishi hivi karibuni ambapo pia ameahidi kuyafanyia kazi maoni ya tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za  haki jinai nchini iliyoongozwa na Mwenyekiti Jaji Mohamed Chande iliyoundwa na  Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Januari 2023.

"Hivi ninavyovifanya wako watu wanafikiri ninafanya mimi tu kwa matakwa yangu, hapana ninafanya haya nimeelekezwa na Mheshimiwa Rais nifanye nini kwamba lazima uhakikishe mahusiano kati ya polisi na wananchi yanakua mazuri,kwamba wananchi wawapende polisi.Leo hii hata polisi akipata shida wananchi wanashangilia nadhani sio sawa maana polisi anatoa huduma kwa wananchi lazima tuboreshe mahusiano" amesema Simbachawene

Ametaja maeneo mawili ambayo ameahidi katika kipindi chake ametumwa kuyafanyia kazi ili kupunguza na kuondoa malalamiko ya wananchi hali inayopelekea wananchi kutotii maelekezo mbalimbali ya serikali.

"Kwanza,mabadiliko ya kimfumo, mabadiliko ya kiutashi kwa mfano mafunzo yetu ya jeshi la polisi lazima tuyaangalie je tunawapa mafunzo ya kwenda kupambana na wananchi au wakawalinde wananchi, wenzetu wale wa tume ya haki jinai, iliyoundwa na Mheshimiwa Rais Dk Samia Suluhu Hassan, wametoa mawazo mazuri sana na rais ameagiza tuyasimamie maoni yao na mimi sasa nitakaa na uongozi wa Juu wa Jeshi la Polisi,tume ya haki jinai wanasema tusiwe na 'Police Force' bali tuwe na 'Police Service' " amesema Simbachawene

"Hatima ya nchi ya Tanzania iko mikononi mwa watanzania, uwe una rafiki yako yuko nje ya Tanzania, uwe unampenda vipi, awe amekusaidia vipi lakini huku Tanzania ndio wako ndugu zako, watoto wako,watanzania wenzako sasa lazima ujue kwamba ipo siku nitahitaji utulivu Tanzania na endapo amani itatoweka tukawa kama nchi za wenzetu,je wewe utakapokua umekaa peke yako moja ya majuto utakayojuta ni kama hukutoa mchango wa kurekebisha hali ikae vizuri na kumbuka katika kurekebisha vizuri sio kutia utambi ili watu waelewe unachosema." amesema Simbachawene.