Kiwanda chafungwa kwa uharibifu wa mazingira

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 04:49 PM Jan 01 2026
Dk Mawazo Nicas
PICHA: JULIETH MKIRERI
Dk Mawazo Nicas

Kiwanda cha Fortune kinachozalisha karatasi kimefungwa kwa muda hadi pale watakapofanya marekebisho kutokana na maji machafu yenye harufu kali ambayo yamekuwa kero kwa wananchi wa karibu na kiwanda hicho.

Kufungwa kwa shughuli za uzalishaji wa kiwanda hicho kumetokana na malalamiko ya wananchi ambao waliyawasilisha kwa Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dk Mawazo Nicas kwenye mkutano wake wa kusikiliza kero kwa wakazi wa Kata ya Misugusugu.

Wakiwa kwenye mkutano uliofanyika mtaa wa vitendo wananchi hao walimueleza Meya kwamba maji machafu kutoka kwenye baadhi ya Viwanda katika eneo la Saeni na Karabaka vimekuwa kero kwa kuharibu mazao kwenye bustani zao.

Mataba Matiku mkazi wa Miyomboni ni kati ya wananchi walioelezea kero hiyo ambaye alieleza kwamba miguu yake ngozi imeathirika kutokana na maji hayo. William Maganga mkazi wa Misugusugu amesema maji hayo machafu na yenye harufu kali yamekuwa kero kwao na hivyo wanahitaji hali hiyo ipatiwe ufumbuzi.

Meya Dk.Nicas alilazimika kufika katika viwanda vinavyolalamikiwa na kushuhudia maji kwenye mabwawa yakiwa na harufu kali machafu kwenye bustani na karibu na makazi ya watu. "Tunawapenda wawekezaji na waendelee kuja kuwekeza kwetu tunachoomba wafuate sheria wazingatie maelekezo ya wataalamu kuondoa malalamiko kama haya," amesema.

Dk.Nicas amesema kuwaacha wawekezaji hao wasifanye marekebisho ni kuwaumiza wananchi wanaoishi na kulima karibu na viwanda hivyo hali ambayo ni hatari kwa afya zao. Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Mrisho Mlela amesema kero kubwa ya uchafuzi wa mazingira imeonekana katika kiwanda cha Fortunate na Radiant.

Amesema wamelazimika kutoa notisi ya siku saba ili wafanye marekebisho, huku kiwanda cha Radiant wakitakiwa kupigwa faini kulingana na uharibifu walioufanya baada ya kukiuka kibali cha mazingira. Akizungumza katika eneo la kiwanda hicho Ofisa Mazingira wa Manispaa hiyo Rahel Ulaya amesema walishatoa penati mara tatu kwa kiwanda hicho sambamba na ilani tatu za marekebisho ambavyo vyote havijafanyiwa kazi.