Mreji wa Mto China uliopo katika daraja linalotenganisha Magomeni Kagera na Mbarahati Mianzini, wilayani Kinondoni, umekumbwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira baada ya takataka mbalimbali kukwama ndani ya mto huo.
Hali hiyo imezua taharuki miongoni mwa wakazi wa maeneo hayo kutokana na hatari za kiafya na kimazingira.
Akizungumza wakati wa tukio la usafi wa mreji wa daraja hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Albert Msando, ameagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na maafisa wa Bonde la Mto Ruvu kusimamia ipasavyo mito na mifereji ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
Msando amesema kwa zaidi ya mwezi mmoja eneo hilo halikufanyiwa usafi, hali aliyosema ni hatari kwa mazingira na usalama wa wananchi, hususan katika kipindi cha mvua. Ameongeza kuwa uzembe katika kufanya usafi wa mara kwa mara huchangia kuziba kwa mifereji na kuongeza hatari ya mafuriko.
Aidha, amebainisha changamoto ya chupa za plastiki, hususan zile zisizonunulika wala kuingia katika mzunguko wa matumizi kama baadhi ya chupa za vinywaji maarufu. Ameeleza kuwa chupa hizo hutupwa ovyo na kuchangia kwa kiasi kikubwa kuziba kwa mito na mifereji.
“Chupa hizi zisizonunulika hazipo katika mzunguko wa matumizi, hivyo husababisha mlundikano wa taka, uchafuzi wa mazingira na hatari ya mafuriko,” amesema Msando.
Katika hitimisho lake, Mkuu wa Wilaya amewahimiza wananchi kubadilika na kushiriki kikamilifu katika kudhibiti taka kwa kuzitupa kwa njia sahihi. Alisisitiza kuwa usafi wa mazingira ni wajibu wa kila mmoja, hasa katika msimu wa mvua, ili kuepusha mafuriko na magonjwa yanayotokana na uchafuzi wa mazingira.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED