Askofu aonya wazazi matumizi ya simu kwa watoto

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 05:07 PM Jan 01 2026


Askofu wa Ufunuo mkoa wa Shinyanga Samawi Allex akizungumza na vyombo vya habari leo, baada ya ibada ya kuliombea Taifa na Rais.
PICHA: SHABAN NJIA.
Askofu wa Ufunuo mkoa wa Shinyanga Samawi Allex akizungumza na vyombo vya habari leo, baada ya ibada ya kuliombea Taifa na Rais.

Askofu wa Kanisa la Ufunuo Tanzania Mkoa wa Shinyanga Samawi Allex, amewataka wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwapatia watoto wao simu za mkononi hususan wanafunzi, akisema zimekuwa chanzo cha watoto kujifunza mambo yasiyoendana na umri wao na hivyo kuchangia kuongezeka kwa uharibifu wa maadili kwa watoto hao.

Askofu Allex aliyasema hayo leo wakati wa ibada maalumu ya kuliombea Taifa na viongozi wake, maombi yaliyofanyika katika kanisa lililopo kata ya Nyasubi Manispaa ya Kahama na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wilaya kutoka katika mkoa huo. 

Alisema ni wajibu wa wazazi na walezi kuhakikisha wanawalinda watoto dhidi ya mmomonyoko wa maadili unaochochewa na matumizi holela ya teknolojia bila uangalizi wa karibu, kwani kinachopatikana ndani ya simu hakiendani na umri wao.

Aidha alisema, simu nyingi zimekuwa na maudhui yasiyofaa kwa watoto, ikiwemo picha na video zisizo na maadili, lugha chafu na mienendo inayowahamasisha watoto kuiga tabia zisizofaa, huku akieleza hali hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa watoto kushindwa kuzingatia masomo yao, kukosa nidhamu shuleni na hatimaye kuacha shule na kujiingiza katika maisha ya mitaani.

Kadhalika aliwahimiza wazazi kuimarisha ushirikiano na walimu pamoja na viongozi wa dini katika kufuatilia mwenendo wa watoto wao ili kuhakikisha wanakua katika misingi sahihi ya hofu ya Mungu, nidhamu na maadili mema na kuongeza malezi yanayoanzia nyumbani ndiyo msingi wa taifa lenye viongozi waadilifu na wananchi wenye uwajibikaji.

Katika ibada hiyo ya kuliombea Taifa na viongozi wake, Askofu Allex aliwaongoza waumini kuliombea taifa liendelee kuwa na amani, umoja na mshikamano huku akiwaombea viongozi wa serikali wa ngazi zote waongoze kwa hekima, uadilifu na hofu ya Mungu.