Tunapoingia mwaka 2026, tutembee na Kristu, tumfanye awe jirani yetu, rafiki yetu, na tufanye sala katika maisha yetu ili atusaidie kutatua changamoto zinazotukabili katika maisha yetu.
Askofu Mkuu wa Jimbo kuu, Katoliki la Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya alisema hayo katika Misa ya mkesha wa kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo iliyoadhimishwa usiku katika Parokia ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba, Jimbo kuu la Dodoma.
Alisema mkifanya hivyo, mtaona vitu vilivyovigumu katika maisha yenu vinapotea. "Pia tunaposherekea sherehe ya kuzaliwa mtoto Yesu, tunatakiwa tufanye kitu kwa wahitaji, jitahidi kutembelea wagonjwa, waone watoto yatima au katembelee magereza, wapelekee zawadi, unapofanya ukarimu kwa wahitaji , hawa masikini na wahitaji ni chombo cha kupata neema kwako, " alisema
Aliomba waumini waliohudhuria ibada hiyo kubeba msalaba wao pamoja na Yesu watapata faraja kwa sababu Yesu pia alipata taabu zote kama wanazozipitia katika maisha yao. "Tumtegemee atatusaidia kutatua changamoto zetu, tuwe na imani atatusaidia, tusimuache, watu wengine wanaamua kujinyonga kwa sababu hawana imani na Yesu," alisema
Alitaja taabu alizopitia Yesu kuwa ni, Yesu alizaliwa kwenye zizi la Ng'ombe sehemu yenye harufu mbaya, amezaliwa familia yenye kipato cha chini, hata kijiji alipozaliwa ni pembeni, siyo kwenye Kasiri ya Kifalme, alisema.
" Nimejiuliza kwanini Mungu alitaka Yesu azaliwe hivyo? alitaka tujifananishe naye, kila mtu ana changamoto zake katika maisha, mwingine anachangamoto kazini, majungu, kijicho, wengine wana changamoto katika ndoa, mtu anagombana na mama mkwe, mawifi, wengine wanasubiri kuolewa bwana haji, wengine sikukuu imefika hawana hela, watu wanapesa zao lakini hawataki kulipa, " alisema.
Alisema, sasa hivi pia Kuna mabadiliko ya tabia nchi, tunapata joto sana, na mwaka 2026 utakuwa siyo mzuri, huyu mtoto Yesu aliyezaliwa atupe faraja katika yale yote tunayopitia, alisema. Aliomba akina baba kukaa nyumbani kwao," ukae nyumbani watoto wakuone, utaenda kutembea kwa rafiki zako siku nyingine, hii ni siku ya familia.
Mbali na hilo alishukuru waumini kumpa zawadi ya Noeli, na kuwambia Mwenyezi Mungu akafanye maajabu katika maisha yao, na awaongezee walipotoa. Misa hiyo iliadhimishwa kwa kushirikiana na Padri Beno Mganga, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba na Padri Saimon Swaga, Wakili Paroko wa Kanisa hilo.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED