Pamoja na kwamba shamrashamra za mwaka mpya zimeshuhudiwa na mamilioni ya watu duniani, sio nchi zote husherehekea mwanzo wa mwaka mpya Januari Mosi.
Taarifa zinaonesha kwamba tofauti za kitamaduni zimesababisha kila jamii kutumia tarehe ya mwaka wao mpya, kulingana na kalenda wanayotumia, kama vile mzunguko wa mwezi au jua, na mila na desturi zao wenyewe.
Hii inatokana na historia na urithi ambao mataifa yamerithi kwa muda mrefu, kila moja ikitegemea mtazamo wake kuhusu mzunguko wa dunia (Jua na Mwezi), na jinsi muda unavyohusiana na dini, mavuno ya kilimo au nguvu za kisiasa.
Aidha, kwa nchi zilizosherehekea leo Januari Mosi, 2026 inamaana zinatumia kalenda ya Gregory ambayo inatambulika kimataifa. Kalenda hii inategemea mzunguko wa jua; na ndiyo inayotumika zaidi duniani ikitajwa kutumiwa na watu wengi duniani.
Inaanza Januari 1. Kihistoria, ilianza katika Milki ya Kirumi, baadaye ikatumiwa na Wakristo na polepole ikapitishwa na nchi zote ulimwenguni.
Kalenda ya Kiislamu (Hijri)
Kalenda ya Kiislamu inategemea mzunguko wa mwezi, ambao ndio unaotumiwa na nchi nyingi za Kiislamu, na mwaka wake huanza na mwezi wa Muharram, mmoja wa miezi mitakatifu ya Uislamu. Kalenda hii ina umuhimu mkubwa katika Uislamu kwa kuwa hutumika kuamua nyakati za ibada kama vile Mfungo wa Ramadhani, Sikukuu ya Iddi, Hija, na matukio mengine ya kidini.
Kalenda ya Hijri ilianzishwa rasmi wakati wa uongozi wa Khalifa Umar bin Al-Khattab (RA) katika karne ya saba BK. Chanzo cha kalenda hii ni tukio la Hijra — kuhama kwa Mtume Muhammad (SAW), kutoka Makka kwenda Madina mwaka 622 BK. Tukio hili linaashiria mwanzo wa dola ya Kiislamu na ndio msingi wa kuhesabu miaka ya Hijri.
Kalenda ina miezi 12, kila mwezi ukiwa na siku 29 au 30, kulingana na kuonekana kwa mwezi mwandamo. Jumla ya siku kwa mwaka ni 354 au 355, hivyo ni mfupi kwa siku 10–11 ikilinganishwa na kalenda ya Gregory (inayotumika kimataifa).
Kutokana na tofauti hii, miezi ya Kiislamu husogea mbele kila mwaka katika kalenda ya kawaida. Miezi iliyopo katika Kalenda ya Hijri ni Muharram, Safar, Rabi‘al-Awwal, Rabi‘al-Thani, Jumada al-Awwal, Jumada al-Thani, Rajab, Sha‘ban, Ramadhani, Shawwal, Dhul-Qa‘dah na Dhul-Hijjah.
Kalenda hii imeainisha miezi minne mitakatifu ambayo ni Muharram, Rajab, Dhul-Qa‘dah na Dhul-Hijjah ambayo inaheshima maalumu na katika historia ya Kiislamu, mapigano yalipigwa marufuku ndani yake isipokuwa kwa sababu za kujilinda.
Waislamu kote ulimwenguni husherehekea mwanzo wa mwaka wa Hijri kwa njia mbalimbali, ikiwa ni pamoja na sala, dua, mikusanyiko na jamaa, na kupamba nyumba kwa mishumaa kama ishara ya upya wa kiroho na ukumbusho wa kuhama kwa Mtume (SAW).
Mwaka Mpya wa Kichina
Watu wa China husherehekea Mwaka Mpya wao kwa kutumia kalenda ya mwezi na jua, ambayo huchanganya mizunguko ya mwezi na misimu ya jua.
Mwaka Mpya wa Kichina hauna tarehe ya kudumu kama ilivyo Januari Mosi, bali huadhimishwa kulingana na kalenda ya mwezi (lunar calendar).
Kwa ujumla, huangukia kati ya tarehe 21 Januari na 20 Februari kila mwaka kulingana na siku ya mwezi mpevu wa kwanza wa kalenda ya Kichina na Wachina husherehekea kwa takribani siku 15 na shamrashamra hizo huhitimishwa na Tamasha la Taa (Lantern Festival).
Kila mwaka huwakilishwa na mnyama mmoja kati ya 12 wa zodiac ya Kichina (mfano Joka au sungura).
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED