ZAIDI ya wakimbiaji 400 kutoka Wilaya ya Moshi wamejitokeza kushiriki mbio za Uru Fun Marathon zenye urefu wa kilometa 5 na 10, zilizofanyika katika eneo la Mingeni, Kata ya Uru Kusini, sambamba na uzinduzi wa taasisi ya Anieli Foundation.
Anieli Foundation inalenga kutoa huduma bure za elimu, mazingira na afya hususan uchunguzi na ushauri wa magonjwa yasiyopewa kipaumbele mara kwa mara, ambayo yanaweza kudhibitiwa kupitia mazoezi na mtindo bora wa maisha.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, aliongoza wakazi hao kushiriki mbio hizo na kufungua rasmi taasisi hiyo iliyoanzishwa kwa heshima ya marehemu Elizabeth Michael Mushi, aliyefariki Oktoba 3 kutokana na kisukari na shinikizo la damu, pamoja na mumewe Anizeth Mushi.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza, Mkuu wa Wilaya Mnzava aliwapongeza waandaaji wa Uru Marathon na familia ya Anizeth Ndetembia Mushi kuona umuhimu wa matukio hayo ambayo yanalenga Kutunza afya.
"Mazoezi ni tiba kubwa dhidi ya magonjwa yakiwemo haya yasiyopewa kipaumbele, lakini tusisubiri mashindano, iwe ni tabia yetu, ofisi yangu kila jumamosi asubuhi imekuwa inashirikisha wadau mbalimbali tunafanya mazoezi,lakini kingine tubadili mfumo wetu wa maisha, tubadili mfumo wetu wa vyakula"Alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Alisema afya imara ni mtaji hivyo ni vyema jamii ikajenga tabia ya kufanya mazoezi hata nyumbani na kupima afya ili kupata faida mbalimbali ikiwemo kuweka afya kuwa njema wakati wote.
Akaahidi Serikali kuendelea kuunga mkono jitihada za wadau wanaofanya kazi ya kuisaidia jamii Kwani ndio kazi ambazo pia Serikali inafanya.
Mwenyekiti Anieli Foundation Gaudence Mushi alisema taasisi hiyo Ina malengo makubwa matatu ikiwemo afya kwa kuhakikisha wanatoa huduma bure za afya ikiwemo upimaji na ushauri kwa magonjwa ya Shinikizo la damu na sukari pamoja na uzito, elimu kwa kusaidia mahitaji kwa watoto wenye uhitaji na utunzaji wa mazingira kwa kuanza na Kata ya Uru kusini na maeneo ya jirani.
Dkt. Phillip Makupa ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya Mawenzi akasema maendeleo ya sayansi, teknolojia na viwanda yamebadili mifumo ya maisha Kwa watu kutotumia nguvu kufanya kazi kama zamani hivyo kusababisha ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, ambayo hayapewi kipaumbele lakini ni hatari Kwa afya.
Akataja magonjwa yanayosumbua jamii kwa sasa kuwa ni Shinikizo la damu ambalo liko Kwa kati ya asilimia 40 hadi 45 kwenye jamii ambapo zamani liliathiri watu wazima wa Umri kuanzia miaka 50 na kuendelea lakini sasa linawagusa Hadi vijana wa kuanzia miaka 30.
Ugonjwa mwingine ni kisukari ambayo licha ya kuwepo kwenye jamii kwa asilimia kati ya 9 hadi 12 tu, lakini Lina madhara makubwa sana hasa kuharibu viungo (organ) za ndani ikiwemo Figo, moyo na ubongo.
Dkt Makupa akasema magonjwa haya licha ya mengine kuchangiwa na vina Saba, akasema sehemu kubwa yanachangiwa na maisha tunayoishi ikiwemo unywaji wa pombe kupita kiasi na sigara,na akasema magonjwa yote hayo yanaweza kudhibitiwa Kwa mazoezi.
Kupitia uzinduzi huo, huduma mbalimbali za kitabibu zilitolewa ikiwemo uchangiaji damu, upimaji wa uzito, kisukari na shinikizo la damu chini ya kaulimbiu “Afya Yako Mtaaji Wako”. Huduma hizo zitakuwa endelevu kila mwaka na zitafanywa Oktoba 03 siku ambayo muasisi wa taasisi ya ANIELI alifariki Dunia.
Mratibu wa Uru Fun Marathon na muasisi wa mashindano hayo, Wakili Wilhad Kitali, alisema mbio ambazo ni msimu wa pili zinalenga kuhamasisha wananchi kushiriki mazoezi na kufurahi pamoja.
Washiriki wote waliokamilisha mzunguko walipewa zawadi za medali huku washindi kuanzia namba Moja hadi tano kwa washindi wa jumla mbio za kilometa kumi na kilometa Tano Tano, kundi la wazee na watoto wmekabidhiwa zawadi za fedha taslimu.
Katibu Tawala wa wilaya ya Moshi, Shaban Mchomvu licha ya kuwapongeza wadhamini mbalimbali kuandaa mbio hizo na hata kufanikisha upimaji afya kwa hiyari alisema mbio hizo zinalenga kuimarisha afya na hazina budi kuungwa mkono na wadau.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED