Klabu ya waandishi Dodoma yanufaika na mafunzo ya EWURA

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:28 PM Dec 31 2025
 Klabu ya waandishi Dodoma yanufaika na mafunzo ya EWURA
Picha:Mpigapicha Wetu
Klabu ya waandishi Dodoma yanufaika na mafunzo ya EWURA

Wanachama wa Klabu ya Waandishi wa Habari mkoani Dodoma, leo Desemba 31, 2025, wameishukuru Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwa kuwapatia elimu kuhusu udhibiti wa huduma za nishati na maji nchini.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Musa Yusuf, ameipongeza EWURA kwa kuandaa mafunzo yaliyolenga kuwawezesha waandishi wa habari kuelewa masuala muhimu yanayohusu mkataba wa huduma kwa wateja, uvunaji wa maji ya mvua pamoja na utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Amesema elimu hiyo itawawezesha wanachama wa klabu kuelimisha umma kwa ufanisi zaidi.

“Asanteni sana EWURA kwa elimu hii. Hakika imetufungua macho, na wenzangu wote ni mashahidi. Tunaomba mafunzo haya yawe endelevu,” amesema Musa.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Wilfred Mwakalosi, amesisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kuwa na uelewa wa masuala yanayodhibitiwa na mamlaka hiyo, akieleza kuwa huduma hizo zinagusa maisha ya kila mwananchi.

“Ninyi waandishi wa habari ni daraja muhimu kati ya EWURA na wananchi. Tuendelee kushirikiana katika kuelimisha umma ili kila mtumiaji wa huduma tunazodhibiti ajue haki na wajibu wake,” amesisitiza Mwakalosi.