Jumla ya watoto 52 walizaliwa usiku wa mkesha wa kuamkia Mwaka Mpya katika Wilaya ya Tarime, mkoani Mara, tukio lililoashiria mwanzo mpya wenye matumaini kwa wakazi wa eneo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Tarime, Dk. Amin Vasomana, alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime walizaliwa watoto 37, wakiwemo wavulana 21 na wasichana 16.
Aliwataka wazazi, hususan wajawazito, kujifungulia hospitalini ili kuachana na imani potofu ya kujifungulia nyumbani, akisisitiza kuwa hatua hiyo huchangia kupunguza vifo vya mama na mtoto aliongeza kuwa matumizi ya dawa za kienyeji wakati wa ujauzito na kujifungua yanaweza kuhatarisha afya ya mama na mtoto kwa kuathiri mpangilio wa uzazi na kuongeza hatari ya vifo, hivyo kuwataka wananchi kuzingatia huduma za kitaalamu za afya.
Wakati huo huo, Muuguzi Mwandamizi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime, Mary Wilson, alisema katika hospitali hiyo walizaliwa watoto watano usiku wa kuamkia Mwaka Mpya, wakiwemo wavulana watatu na wasichana wawili, huku watoto wote wakiwa salama alieleza kuwa kati ya waliojifungua, watatu walijifungua kwa njia ya kawaida na wawili walifanyiwa upasuaji.
Muuguzi huyo aliwasisitiza wazazi kuzingatia ratiba za kliniki, kuwanyonyesha watoto maziwa ya mama, kuwapa chanjo kwa wakati na kuhakikisha wanapata lishe bora ili kuwakinga dhidi ya upungufu wa virutubisho , huduma hizo ni muhimu kwa afya na ustawi wa mtoto tangu anapozaliwa.
Baadhi ya akina mama waliopata watoto siku hiyo Rebeka William, mkazi wa Somba Nyasoko wilayani Rorya na Esther Chacha, mkazi wa Tagota, walimshukuru Mungu Kwa kwawajalia afya njema na kufanikiwa kuingia mwaka mpya wakiwa na watoto wao .
" Tunawashukuru pia watoa huduma katika hospital hii wametuhudumia vizuri nawahimiza wanawake wenzangu kutokuwa na hofu ya ujauzito na kujifungua, akisema mtoto ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu." Alieleza William
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED