Katika kuelekea Sikukuu ya Mwaka Mpya, Serikali imepiga marufuku matumizi ya fataki na uchomaji wa matairi, ikieleza kuwa vitendo hivyo vinaweza kusababisha taharuki na kuvuruga amani katika jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amewataka wakazi wa mkoa huo kuwa mabalozi wa amani katika kipindi cha sikukuu. Amesisitiza kuwa wananchi hawapaswi kupiga fataki bila kupata kibali cha mamlaka husika, kwani hali hiyo inaweza kuleta mshutuko na hofu kwa wananchi wengine.
Ameongeza kuwa serikali inaendelea kutoa elimu ya ulinzi na utunzaji wa amani ili kuhakikisha mkoa haurudii katika hali zisizoridhisha, huku akiwataka wananchi kuwa wadau wema katika masuala ya amani na usalama. Amesisitiza kuwa haki na amani haviwezi kutenganishwa, na kila mmoja anatakiwa kutimiza wajibu wake.
Aidha, Mkuu wa Mkoa amewaomba viongozi wa dini kuhubiri amani katika kipindi hiki cha sikukuu ili kujenga Mkoa wa Dar es Salaam unaozingatia misingi ya amani na mshikamano wa kijamii. Amehimiza wananchi kusherehekea sikukuu kwa amani bila kunyang’anya mali za watu, kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani na kutoeneza chuki au udini, ili kuhakikisha mkoa unaendelea kuwa salama na wenye utulivu.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED