CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetuma salamu za heri ya Mwaka Mpya kwa Watanzania, kikisema mwaka 2026 unapaswa kuwa mwanzo wa uponyaji taifa kwa kujengwa juu ya misingi ya ukweli, haki na uwajibikaji wa kweli.
Salamu hizo zilitolewa juzi jioni na Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara, John Heche, aliyesema taifa linaingia Mwaka Mpya likiwa limebeba maumivu, hofu na uchovu uliowagusa wananchi wengi kutokana na changamoto mbalimbali za kijamii, kisiasa na kiuchumi.
"Tunapoingia Mwaka Mpya, tunatambua maumivu, hofu na uchovu uliowagusa wananchi wengi. Tunawatakia uponyaji mioyo, faraja kwa waliopoteza wapendwa wao pamoja na matumaini mapya kwa kila kijana, mkulima, mfanyabiashara na kila familia ya Kitanzania," alisema Heche.
Akinukuu maandiko matakatifu, Heche alisema faraja na tumaini ni nguzo muhimu katika safari ya kuponya taifa, akisisitiza kuwa jamii yenye majeraha ya kihisia na kijamii inahitaji haki na ukweli ili kurejesha imani na mshikamano wa kitaifa.
"Kama maandiko matakatifu yanavyotukumbusha, "Bwana yu karibu na waliovunjika mioyo, huokoa waliopondeka roho'," alisema.Hata hivyo, Heche alisisitiza kuwa taifa haliwezi kuponywa kwa maneno matamu pekee bila kukiri makosa na kushughulikia mizizi ya matatizo yanayolikabili.
"Amani ya kweli haiwezi kujengwa juu ya uongo, hofu au kuficha ukweli. Maridhiano ya kweli huanza pale mamlaka inapokiri ukweli, kuwajibika na kurejesha haki kwa waliodhulumiwa," alisema, akiongeza kwa kunukuu Qur’ani Tukufu: "Hakika Mwenyezi Mungu hawabadilishi hali ya watu mpaka wabadilishe yaliyo ndani ya nafsi zao."
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho anatarajiwa kuhutubia taifa kesho Januari 3, ambapo atazungumzia kwa kina masuala ya msingi yanayolikabili taifa, msimamo wa chama hicho na wito wa mabadiliko ya haki kama nguzo ya amani ya kudumu nchini.
Kauli ya CHADEMA inakuja wakati taifa linaanza Mwaka Mpya likiwa na mjadala mpana kuhusu maridhiano, haki na mustakabali wa amani ya kudumu. Tayari Rais Samia Suluhu Hassan kupitia hotuba yake ya kufunga mwaka 2025 na kuukaribisha Mwaka Mpya 2026 juzi usiku, alisema mchakato wa kuunda Tume ya Maridhiano unaendelea.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED