Mbunge Sigrada Mligo aja na mpango kusaidia wenye ulemavu

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 02:32 PM Jan 02 2026
Mbunge Sigrada Mligo aja na mpango kusaidia wenye ulemavu
PICHA: ELIZABETH JOHN
Mbunge Sigrada Mligo aja na mpango kusaidia wenye ulemavu

Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Njombe kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Sigrada Mligo, amesema ana mpango wa kuwasaidia watu wenye ulemavu katika mkoa huo kwa kuwatafutia mitaji ya kujikwamua kiuchumi pamoja na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Sigrada ametoa kauli hiyo mara baada ya kushiriki hafla ya chakula cha mchana cha pamoja kwa ajili ya kufurahia mwaka mpya na baadhi ya watu wenye ulemavu, hafla ambayo pia ililenga kusikiliza kero na maoni yao. Amesema kuwa ameahidi kutafuta wadau watakaosaidia kutoa mitaji kwa watu wenye ulemavu, akisisitiza kuwa mahitaji yao ya mitaji si makubwa kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu.

“Nimeahidi kutafuta wadau kwa ajili ya kuwasaidia mitaji kwa sababu mahitaji yao si makubwa. Sio kweli kwamba kila mmoja anahitaji mtaji wa milioni tano; wapo wanaojishughulisha na shughuli ndogo ndogo kama kutengeneza unga wa lishe,” amesema Sigrada.

Aidha, Sigrada amesema uamuzi wake wa kuwafikia watu wenye ulemavu umetokana na kutafakari kwa kina changamoto wanazopitia katika maisha yao ya kila siku. Ameahidi pia kushughulikia changamoto za kisera zinazowahusu kupitia Bunge mara baada ya vikao vya Bunge kuanza.