Shinyanga mkoa wa mfano janga la athari za tabianchi

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 10:06 AM Dec 26 2025
Shinyanga mkoa wa mfano janga la athari za tabianchi
PICHA: MARCO MADUHU
Shinyanga mkoa wa mfano janga la athari za tabianchi

Shinyanga ni moja ya mikoa ya mfano linapokuja suala la maeneo yaliyoathiriwa pakubwa na mabadiliko ya tabianchi kuna mifano michache tu kati ya mingi na hii ni ya mwezi huu pekee. Desemba 12, 2025, zaidi ya nyumba 200 wilayani Kahama ziliangushwa na mvua iliyoambatana na upepo mkali, hali iliyosababisha wananchi kukosa makazi.

Aidha, katika Wilaya ya Shinyanga, kulitokea maafa kama hayo yaliyosababisha kifo cha mtu mmoja baada ya nyumba kuanguka. zinaweza kuwapo kwa sababu nyingi, lakini kubwa na isiyo na shaka ni hii ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Hilo linathibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro anasema maafa ya mvua na upepo yanayotokea mara kwa mara yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na maeneo mengi ya makazi ya wananchi kukosa miti.

“Desemba 12, mvua kubwa ilinyesha hapa Shinyanga ikiambatana na upepo mkali, nyumba nyingi zilianguka na kusababisha kifo cha mtu mmoja, chanzo kikubwa ni maeneo mengi kutokuwa na miti,” anasisitiza Mtatiro.

Anasema Serikali imekuwa ikiendesha kampeni za upandaji miti kila kaya kwa kushirikiana na taasisi za umma na kwamba kampeni hizo zitaendelea ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mmoja wa wakazi wa Shinyanga, Jilala Duttu mkazi wa Ibanza amesimulia yaliyowasibu katika janga la mvua, anasema mvua ilianza kunyesha majira ya saa tisa usiku ikiwa na upepo mkali, na ghafla mabati yakaanza kuezuliwa na kisha nyumba kuanguka.

“Nyumba ilipo anguka Mtoto alipigwa na tofali kichwani akajeruhiwa, huku mama mkwe akivunjika mguu, lakini tunashukuru wote wako hai,” amesema Dutu.

Katika kukabiliana na athari hizo, Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Shinyanga, Ezra Manjerenga anasema kupitia kampeni ya mkuu wa wilaya ya upandaji miti, kwamba kuanzia Julai 2024 hadi Juni 30, 2025, jumla ya miti 994,213 ilipandwa na kati ya miti hiyo, 705,891 iliota na 208,784 ilikufa kutokana na kutotunzwa na mingine kuliwa na mifugo.

“Wananchi wa Shinyanga bado wako nyuma katika suala la upandaji na utunzaji wa miti, idadi kubwa ya miti iliyokufa ni matokeo ya kutotunzwa ipasavyo,” amesema Manjerenga.

Anatoa ahadi kuwa, Serikali itaendelea kuhamasisha wananchi kupanda miti, na kutoa elimu ya umuhimu wa uhifadhi wa mazingira na kuacha ukataji miti hovyo.

Ofisa Mwandamizi wa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Wilaya ya Shinyanga, Fabian Balele anasema kwa kiasi kikubwa, ukataji ovyo wa miti unachochewa na biashara ya mkaa.

Anasema ofisi yake imeweka mikakati ya kutafsiri kwa vitendo Sheria ya Misitu Na.14 ya mwaka 2002 na kanuni zake ili kudhibiti shughuli za uuzaji mkaa kiholela.

“Ukataji miti ovyo ni chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi, kila siku tunakamata watu kati ya sita hadi saba wanaojihusisha na biashara haramu ya mkaa, tunawatoza faini na kutaifisha mali zao,” amesema Balele.

Ofisi yake haiishii kukamata na kutaifa pekee, Balele anasema imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa na kwamba mkakati huo ni endelevu.

“Mwakani 2026 , TFS Shinyanga tunatarajia kuwa na mashine za kuzalisha mkaa mbadala ambao unatokana na malighafi zingine na siyo miti. Pia, tutatoa mafunzo bure kwa wananchi juu ya namna ya kutengeneza mkaa huo. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba wanaachana kabisa na kuni na mkaa,” amesema Balele.

Sambamba na mkakati huo, anasema TFS inaotesha miche milioni moja ya miti kila mwaka. Akitoa mfano anasema kwa mwaka huu, taasisi hiyo ya Serikali imeotesha miche 600,000 katika Bwawa la Ninghw’a na kuigawa bure kwa wananchi na taasisi za serikali.

“Miti huwa ina tabia ya kufyonza hewa ukaa, ambayo ni kaboni, hivyo ikipandwa kwa wingi itasaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Ndio maana tumekuwa tukihamasisha wananchi kupanda miti.” amesema Balele

Mwenyekiti wa kundi la majadiliano la Afrika kuhusu mabadiliko ya tabianchi (AGN), Dk. Richard Muyungi anasema kupitia mkutano wa COP30 uliofanyika Belem huko Brazil, Tanzania imeteuwa watu sita watakaoingia kwenye kamati mbalimbali za kimataifa zinazohusu maamuzi ya masuala ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Hii ni hatua kubwa kwetu kama nchi, si jambo rahisi nchi kufanikiwa kuingiza wataalamu sita, kwenye kamati mbalimbali za dunia zinazosimamia masuala ya mabadiliko ya tabianchi,” anasema Dk. Muyungi.

Anasema moja ya ajenda ambayo Tanzania imeibeba katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ni suala la nishati safi ya kupikia pamoja na mpango mkakati wa Taifa wa Nishati Safi (NCCS 2024–2034), ambao umelenga kuongeza upatikanaji wa asilimia 80 wa nishati safi ifikapo 2034.

Mkakati huo utasaidia kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kwa kuwa hakutakuwa na ukataji wa miti ovyo ambao ndicho chanzo kikubwa cha athari za mabadiliko ya tabianchi, kama matukio hayo ya mvua kubwa zilizosababisha majanga ikiwamo kifo katika wilaya za Kahama na Shinyanga.