OMO: Safari hii hatutakubali kura ya siku mbili Zanzibar

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:45 PM Dec 09 2024
Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman.

Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Taifa, Othman Masoud Othman, amesema chama hicho hakitakubali Zanzibar kufanyika kura ya siku mbili.

Othman,  ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo Jumatatu Desemba 09  2024, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la Vijana wa ACT-Wazalendo wa Mkoa wa Kati Kichama, huko katika Ukumbi wa Chama hicho, Dunga Mkoa wa Kusini Unguja.

"Wajibu wetu ni kuilinda Katiba ya Zanzbar; kama ambavyo tuliahidi katika Kiapo, ili  kupambania haki na kuwahudumia wananchi;  hivyo tunaahidi 'Kura ya Mapema' haitojirudia Zanzibar".

Aidha Othman amesema ACT siyo wakala wa ajira kama wafanyavyo vyama vyengine, bali dhima yake kuu ni kupigania haki na maslahi ya watu wote, bila ya ubaguzi. Amewahimiza Vijana kuacha kughilibiwa na  kudanganywa, kwa kivuli cha kupewa ajira, na  badala yake wasimame imara kutekeleza dhamira ya kuitafuta Zanzibar yenye Mamlaka Kamili.

Wakitoa salamu zao, Katibu wa Taifa wa Vijana, na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Mkoa wa Kichama wa Kati, wa Chama hicho, Muhamed Khamis Busara, na Suleiman Ali Seif, kwa nyakati tofauti wamesema kuwa, 2025 ni Mwaka wa Maamuzi na wa mabadiliko, ambapo vijana kwao ni wajibu kuwepo  mstari wa mbele katika kulifanikisha hilo.

Kongamano hilo ni mwendelezo wa Makongamano ya Ngome ya Vijana yanayoendelea, na yanayotarajiwa kufanyika Nchini kote, likibeba Kaulimbiu ya "Nafasi ya Vijana kuelekea Uchaguzi 2025 na Ukombozi wa Zanzibar"

Viongozi wa Ngazi mbali mbali wa Chama hicho,  wamehudhuria Hafla hiyo, wakiongozwa na Katibu wa Habari na Uenezi Taifa, wa ACT-Wazalendo,Salim Abdallah Bimani.