Pacha walioungana watenganishwa, kukaa Muhimbili mwaka mmoja

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 10:57 AM Dec 10 2024
Pacha walioungana watenganishwa, kukaa Muhimbili mwaka mmoja

WATOTO mapacha Hussein na Hassan Jumanne (3), waliokuwa wameungana baadhi ya viungo vya mwili, ikiwamo kibofu cha mkojo na utumbo, wamerejea nchini wakitokea Saudi Arabia, walikokaa kwa mwaka mmoja na miezi minne kwa ajili ya kutenganishwa.

Hussein na Hassan, waliondoka nchini Agosti 23, mwaka jana, kwenda kufanyiwa upasuaji Oktoba 5, mwaka jana, na iliwachukua madaktari saa 16 kuwatenganisha katika hospitali ya King Abdulaziz, iliyoko Riyadh, Saudi Arabia.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk.  Rachel Mhavile, akizungumza jana, jijini Dar es Salaam katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), alisema kutokana na watoto hao kuzaliwa wakiwa viungo vimeungana sehemu tatanishi, ililazimika kupelekwa nchini huko.

“Tumekuja kuwapokea watoto, pamoja na mama yao waliokaa Saudi Arabia kwa takribani mwaka mmoja, kabla walikaa MNH mwaka mmoja na zaidi wakisubiri kukua na kuwa katika hali nzuri kwa ajili ya kwenda kwa wenzetu kusaidia matibabu,” alisema Dk. Mhavile.

Alieleza kuwa awali, Hadija alipojifungua alipatiwa huduma zote MNH, lakini ilipofika suala la kuwatenganisha wadau wengine walihitajika. “Haya ni matibabu ya awamu ya kwanza ya kuwatenganisha, sasa tunarudi nao MNH tunawapa nyumba ya kuishi mojawapo kwa mwaka mzima tena na baada ya mwaka watarudi tena Saudi Arabia.

"Upasuaji wa hawa watoto walioungana huwa inategemeana wameungana sehemu zipi, wakiwa wameungana maeneo ambayo ni ‘complex’ au tata kama moyo, uti wa mgongo, sehemu za siri au wanajumuika miguu.

“Kwa mfano, hawa walikuwa na miguu mitatu. Kila mmoja ana mguu imara ila ule wa tatu haujaimarika, ilihitaji ubingwa zaidi ambao sisi bado tunauhitaji, Saudi Arabia, imekubali kutusaidia, lakini bado wa kwetu wanajifunza,” alisema Dk. Mhavile.

Dk. Mhavile ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji MNH, alisema pia mapacha hao watakaporejea Saudi Arabia watapatiwa mguu wa pili wa bandia kila mmoja, baada ya mguu wa tatu kuondolewa ambao ulikuwa dhaifu.

Bingwa wa Upasuaji wa Watoto MNH, Dk. Zaitun Bokhary, alisema upasuaji wa watoto hao ulifanyika jijini Riyadh, Oktoba 5, mwaka 2023 kwa saa zipatazo 16 ukiwashirikisha wataalamu mbalimbali wakiwamo mabingwa wa watoto, mifupa, kibofu cha mkojo na mishipa ya fahamu na damu.

“Watoto hawa waliungana kuanzia kifua, tumbo, nyonga, waliungana kwa ndani utumbo mkubwa na baadhi ya mishipa ya damu iliungana na eneo lililokuwa tatanishi zaidi ni kibofu cha mkojo. Mmoja kilikuwa wazi kwa nje, mwingine kilikuwa kimefunika wa ndani, ni eneo tata, lililohitaji kuhusisha mabingwa wa kibofu cha mkojo wasiopungua wanane.

Pia, madaktari bingwa wa mifupa walihitajika kuutenganisha mguu wa tatu na kuuondoa, sasa wote wana mguu mmoja mmoja, kituo walikofanyiwa upasuaji wana uzoefu wa upasuaji wa aina hii na wamebobea kwa miaka zaidi ya 30,” alisema D. Zaitun.

Hadija Shaban (24), mama wa watoto hao aliishukuru serikali pamoja na Saudi Arabia, kwa kuwa akiwa nchini humo iliwagharamia kuanzia matibabu pamoja na huduma zote za mlo na malazi.

“Mimi ndio baba, ndio mama, MNH ndio ndugu zangu, wa kwangu hawajwahi kutokea hata siku moja, na Dk. Zaitun, ni mama yangu, Mungu amzidishie. Nilipotoka Igunga, Tabora hadi kwenda Saudi Arabia, alinisaidia hata katika kuwasiliana nikiwa huko kwa sababu binafsi sijui lugha ya Kiarabu wala Kiingereza,” alisema Hadija.

Kadhalika, Hadija aliomba msaada wa kupatiwa uwezeshaji wa makazi kwa kuwa atahitajika kukaa mkoani Dar es Salaam, wakati akiendelea na matibabu kwa zaidi ya mwaka mmoja.