WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 itazingatia misingi ya umoja, utu, uhuru, haki, demokrasia, ulinzi wa maliasili, rasilimali, utamaduni na maadili ya taifa.
Waziri Kitila amebainisha hayo leo mkoani Dar es Salaam, wakati wa mkutano wa vyama vya siasa na Tume ya Mipango, akieleza kuwa misingi hiyo itatakiwa kuzingatiwa na watu wote ikiwamo wanasiana na vyama vya kisiasa.
Amesema serikali imeamua kukutana na viongozi wa vyama vya kisiasa kwakuwa ni wadau wakuu wa ulinzi wa misingi hiyo, akisisitiza kuwa dira hiyo inanuia pia kuifanya Tanzania kuwa taifa la demokrasia likiongozwa na katiba imara inayoakisi muafaka wa kitaifa, taasisi madhubuti za umma na mfumo thabiti wa vyama vya siasa.
"Agosti mwaka huu, wakati wa kutoa maoni yao kuhusu dira 2050, vyama vya siasa vilitaka elimu kupewa kipaumbele, kuwekewa ulinzi wa kisheria, kujengwa taifa lenye demokrasia na haki, matumizi ya teknolojia katika uzalishaji, matumizi bora ya rasilimali ikiwemo ardhi pamoja na ugatuzi wa madaraka katika utawala na uwezeshaji wa vijana nchini," amesema Prof. Kitila.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED