RIPOTI MAALUM: Hatari ulaji kuku vifaranga

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 09:59 AM Dec 22 2024
Biashara ya kuku
Picha: Mtandao
Biashara ya kuku

KUKU wa kisasa ni moja ya vitoweo vinavyopendwa katika maeneo mbalimbali nchini. Katika sehemu mbalimbali, watu wamekuwa wakitumia kitoweo hicho kikiwa kimechomwa au kukaangwa sambamba na vyakula vingine kama ugali na chipsi. Matumizi makubwa yamekuwa katika vibanda vya chipsi au migahawa.

Pamoja na umaarufu na kupendwa na watu wengi, wataalamu wanaonya endapo wafugaji hawatazingatia taratibu za ufugaji, kuna madhara makubwa ambayo yatampata mtumiaji, ikiwamo kutengeneza usugu wa dawa kwa binadamu.

Wanasema kuku huwa tayari kwa matumizi wanapofikisha umri wa kuanzia mwezi mmoja na kuendelea lakini kwa sasa baadhi ya wafugaji huwaingiza sokoni wakiwa na umri wa chini ya wiki tatu tangu walipoanguliwa vifaranga.

Uchunguzi wa Nipashe katika masoko mbalimbali mkoani Dar es Salaam yakiwamo ya Shekilango na Mwananyamala, umebaini asilimia kubwa ya kuku wa kisasa hupokewa tayari kwa kuuzwa wakiwa bado ni vifaranga ambao hawajatimiza mwezi, kama wataalam wa mifugo wanavyoshauri.

Nje ya masoko hayo,  wahitaji wengi wa kuku ni pamoja na mama lishe na wakaanga chipsi, ambao asilimia kubwa ya watu huwategemea katika mlo mmojawapo wa siku.

Amina Said, mama lishe aliyekutwa katika soko la Shekilango akinunua kuku, anakiri hali ya kuku wanaoingizwa sokoni hivi sasa hawastahili kwa ulaji kwa sababu ni wadogo, wanapowanyonyoa huwa kama ndege.

“Wateja wetu wanalalamika wanaona kama tunawauzia kuku wadogo, lakini bei ya chakula haijabadilika ipo palepale. Ushauri wetu wafugaji wahakikishe kuku wanayemleta sokoni angalau basi awe na miezi miwili na kuendelea,” alishauri.

Anthony Lyimo, mkaanga chipsi ambaye alikutwa soko la Mwananyamala akinunua mahitaji yake, wakiwamo kuku, alishauri wizara husika (ya Mifugo na Uvuvi),  kutoa elimu kwa wafugaji ili kuepuka kupeleka sokoni kuku wakiwa vifaranga.

“Tunachouziwa sokoni ni vifaranga, vingine havieleweki. Unajiuliza  ni wazima kweli? Halafu kwa umri chini ya mwezi wanakuwa kwenye hatua ya kukuzwa na dawa mbalimbali. Hatujui  ulaji wa kuku wa aina hii athari zake kwa binadamu ni zipi. Chipsi kuku ni Sh. 3,500 na kwingine 4,500. Wateja  wanalalamika kuwa kuku ni wadogo,” anasema.

Hamisi Ramadhani, mfanyabiashara wa kuku katika soko la Shekilango, anasema wanalazimika kuwachukua kuku hao kabla ya muda unaotakiwa kuingizwa sokoni kwa sababu upatikanaji wake kwa sasa ni wa shida. Anasema kuna wakati wanakosa hata kuku mmoja wa kuuza huku uhitaji sokoni ukiwa mkubwa, 

“Wafugaji wanatupigia simu wanauza kuku wakiwa na wiki tatu. Kutokana na uhitaji sokoni, tunalazimika kuwachukua ili wakulie hapo sokoni  lakini wateja wakija wanawataka vivyo hivyo.

“Ninauza kuku lakini ninanunua huko shamba la Bagamoyo kwa wafugaji. Kwa  mfano leo (juzi) kuku wameadimika sana. Ukienda  shambani ukiacha kuchukua kwa kuwa hawajatimiza muda, unakuta mwingine kachukua,” anasema.

Mfanyabiashara mwingine, Juma Mlupili, anasema kinachosababisha kuadimika kwa kuku na kufanya kuuzwa  kabla ya muda ni kupanda kwa bei za vyakula. Anasema kuku hao wanapofika wiki tatu wafugaji huwapigia simu na kuwauza kwa sababu wanakimbia gharama za ufugaji wanazodai kwa sasa ni kubwa.

“Inawezekana sababu ikawa kupanda kwa bei za vyakula, wafugaji wanauza mapema ili wapate faida wasiendelee kuwalisha mpaka watimize muda wa kitaalamu,”anasema.

Mlupili anataja sababu nyingine kuwa ni msimu huu wa sikukuu mahitaji ya kuku hayo yanaongezeka kwa kuwa wafugaji wengi hasa wachaga wanakwenda kula sikukuu  mkoani.

“Inawezekana pia wafanyabiashara wamehifadhi kuku ndani waje kuwauza siku ya sikukuu, maana wengi wanavizia siku hiyo wakijua kuwa  bei itakuwa juu wapate faida zaidi,” anasema.

KAULI YA WAFUGAJI

Mfugaji wa Kuku kutoka Mapinga, Bagamoyo mkoani Pwani, Musa Jackson, anasema kinachosababisha wauze kuku kabla ya muda ni gharama kubwa za chakula cha kuku. Anasema watu wengi wanaacha kujihusisha na biashara hiyo wameona hawapati faida kutokana kuongezeka kwa gharama za dawa na chakula cha kuku.

“Kwa mfano pumba ya kuku mwaka juzi gunia lilikuwa Sh. 20,000 sasa hivi ni Sh. 32,000 na ukiangalia hakuna dalili za kushuka kwa hizo gharama. Hata gharama za dawa za kutibu kuku na za madaktari wanaopima kuku nazo zimepanda na kusababisha uendeshaji kuwa juu.

“Serikali iweke bei elekezi kwa vyakula vya kuku ili kusaidia wafugaji wapate vyakula kwa bei inayofanania maana maduka mengine yanauza kwa gharama kubwa sana hali inayokatisha tamaa,” anasema.

Mfugaji mwingine kutoka Kivule, Dar es Salaam, Msafiri Ngonyani,  anaungana na Jackson akisema gharama za vyakula vya kuku kuwa juu ndiyo sababu ya wao kuuza kuku  wakiwa chini ya muda.

“Kuku anapokaa kwa muda mrefu anatumia chakula kingi na gharama kubwa. Ukija  kupiga hesabu ukimuuza kwa Sh. 5,500 hupati faida. Kwa hiyo kinachotokea mfugaji anatangaza anauza kuku hata kama hawajafikisha muda ili asiendelee kupata gharama,” anasema.

Ngonyani anasema baadhi ya mbegu za kuku hao wa kisasa mbegu zao zimedumaa hata akifika wiki nne bado ataonekana mdogo.

MADHARA MWILINI 

Mganga wa mifugo, Dk. Allen Audax, anasema kwa ufugaji wa Kitanzania, kuku  wanakuwa tayari kwa matumizi wanapofikisha umri kuanzia mwezi mmoja na kuendelea.

Anasema kuku aliye chini ya wiki nne, wakati mwingine anakuwa bado anatumia dawa, hivyo akiuzwa na mtu akala maana yake atakuwa anakula dawa iliyokuwa ndani ya kuku huyo.

Pia anasema katika kila dawa anayopewa kuku, kuna maelekezo ya kuwa anaweza kuliwa kwa muda fulani baada ya kupewa dawa hiyo na kwamba akiliwa kabla ya muda wa maelekezo kwisha, mlaji anakuwa amekula na dawa iliyo ndani ya kuku.

“Kwa hiyo kama mtu akiwa ana tabia ya kula  kuku ambao bado dawa hazijaisha ndani ya miili yao, ina maana dawa za kuku zitakuwa zinaingia mwilini mwake. Matokeo yake mwili wake utakuwa unatengeneza mazoea ya dawa, hivyo siku akija kuumwa na kutumia dawa za binadamu zinaweza zisifanye kazi,” anasema.

Dk. Audax alibainisha kuwa kuku wakiwa hawajakomaa wanakuwa na upungufu wa protini  na mafuta kulinganisha na kuku waliofikia umri kwa kuuzwa, hivyo mtu akila anakosa virutubisho muhimu.

Pia anasema pia kuku hao wakiwa chini ya umri wa kuuzwa wana upungufu mkubwa wa ladha kwa sababu ya upungufu wa protini na mafuta  kwenye nyama zao.

Daktari Bingwa wa Tiba ya Familia kutoka Hospitali ya Aga Khan, Willbroad Kyejo, akizungumza kitaalam madhara ya usugu wa dawa kwenye mwili wa binadamu, aanasema kunakuwa na ugumu wa kutibu  magonjwa  kwa sababu dawa atakazokuwa anatumia mgonjwa haziwezi tena kuua bakteria wanaosababisha ugonjwa. 

"Kwa mfano, mtu akipata homa ya mapafu, dawa za kawaida zinaweza kushindwa kufanya kazi na mgonjwa anaweza kuendelea kuwa mgonjwa au hata kufariki dunia," anasema.

Dk. Kyejo alisema pia gharama za matibabu zinaongezeka kwa sababu mwili ukiwa sugu kwa dawa za kawaida, mgonjwa atahitaji dawa za gharama kubwa zaidi au matibabu ya muda mrefu jambo linaloongeza mzigo wa kifedha kwa familia na taifa.

“Madhara mengine ya usugu wa dawa ni mgonjwa kupoteza maisha  kwa sababu magonjwa sugu hayawezi kutibika kwa urahisi. Wagonjwa  wengi zaidi wanaweza kupoteza maisha, hata kwa maambukizi ya kawaida,” anasema.

Pia anasema husababisha maambukizi kuenea kwa urahisi  kwa mtu mmoja hadi mwingine, hasa katika maeneo yenye watu wengi kama hospitalini, shuleni au nyumbani.