JUKWAA la wanaharakati wa kupambana na ukatili wa kijinsia mkoani Kilimanjaro, limefichua siri kuwa migogoro mingi ya ndoa inayoibuka kila uchao mkoani humo, inasababishwa na baadhi ya wanawake ambao vipato vyao vimeimarika, kutokuwa na heshima katika ndoa.
Huku, wanawake hao wakiwa hawaoni sababu ya kushiriki tendo la ndoa na wenza wao.
Msemaji wa mashirika 12 ya kiraia yaliyotoa tamko la kulaani ukatili huo, Wakili mkongwe nchini na mwanaharakati wa haki za binadamu, Elizabeth Minde, alisema kundi rika la miaka 30 hadi 45 ya wanawake wameonekana kulalamikiwa sana maeneo mbalimbali.
“Wengine wakisema, ‘hawa wapora wadogo (mke mdogo) wanawaonea sana waume zao’ mfano halisi ni nukuu kutoka katika mjadala wa kijamii uliofanyika Kata ya Mwika Kaskazini.
“Sisi wanaharakati tunasema kuwa kuimarika kwa kipato cha mwanamke kisiwe chanzo cha migogoro ya ndoa. Muhimu ni kuimarisha mawasiliano, mahusiano na maamuzi shirikishi katika bajeti za familia, matumizi ya muda kwa uwazi na uwajibikaji wenye ustawi chanya na ulioendelevu ndani ya familia.”
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED