TANZANIA ni moja ya nchi yenye vitu vingi vinavyoshangaza na wakati mwingine huchochea mijadala ambayo inazidi kuitangaza kiutalii na kuvutia watafiti na watalii.
Mfano wa maajabu ni kuhama kwa nyumbu kutoka mbuga ya Serengeti kuelekea nchi jirani ya Kenya kwenye hifadhi ya Maasai Mara wakati wa kupata mimba, lakini pia hurudi na kuzalia Serengeti.
Pamoja na hilo ipo hifadhi ya Ngorongoro Creter ambayo ni moja ya maajabu ya dunia ambayo ni makazi ya binadamu na wanyamapori, bila kuwa na matatizo.
Hivi karibuni kuna tukio ambalo limesababisha wanasayansi kuanza kufanya utafiti baada ya samaki mkubwa nyangumi kusafiri kwa umbali mrefu kutoka Bahari ya Pasifiki nchini Colombia hadi Tanzania akitua ndani ya Bahari ya Hindi.
Columbia iko bara la Amerika Kusini ambalo ni mbali mno kwa safari ya kiumbe huyo.
Nyangumi huyo mwenye nundu anadaiwa ndiye samaki wa aina hiyo aliyefanya uhamaji wenye masafa marefu zaidi na ya kipekee ambayo hayajawahi kurekodiwa.
Wanasayansi ambao wanachunguza safari hiyo ya nyangumi, wanaeleza huenda umechochewa na mabadiliko ya tabia nchi.
Nyangumi huyo alionekana katika Pasifiki karibu na Colombia mwaka 2017, kisha alikutwa tena miaka kadhaa katika Bahari ya Hindi kisiwani Zanzibar, umbali wa kilomita 13,000.
Katika utafiti uliochapishwa na jarida la sayansi, la Royal Society Open Science, wataalam wanaamini kuwa safari hiyo ndefu inaweza kuwa imesababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Mabadiliko ya tabianchi yanachangia kupungua kwa hifadhi za chakula au safari ya kutafuta wenza.
Ekaterina Kalashnikova kutoka kwa programu ya mamalia wa baharini Tanzania, anasema kwamba tukio hilo ni la kushangaza na la kipekee hata kwa aina hiyo ya wanyama wanaohama.
Dk.Kalashnikova anasema kuwa kuna uwezekano kuwa umbali aliosafiri ni mrefu zaidi kuwahi kurekodiwa kwa nyangumi mwenye nundu.
Hata hivyo, aina hiyo ya nyangumi wenye nundu huishi katika bahari zote duniani.
Pia husafiri umbali mrefu kila mwaka na wanahama kwa umbali mrefu kuliko mamalia yoyote, wakisafiri kutoka maeneo ya kitropiki ambayo wanapozaliana maeneo yenye chakula katika maji baridi.
Lakini safari ya nyangumi huyo dume ilikuwa ya kipekee zaidi, ikiwa na maeneo mawili tofauti ya kuzaliana.
Nadharia moja ni kwamba mabadiliko ya tabia nchi yanabadilisha wingi wa uduvi kamba wadogo wanaoliwa na nyangumi hivyo kuwalazimu kuhamia bahari tofauti kutafuta chakula hicho.
''Ingawa sababu halisi bado hazijabainika, lakini uhamaji wa nyangumi wenye nundu huenda unachochewa na mabadiliko ya tabianchi, mazingira mabaya ambayo yanatokea kila wakati na mabadiliko ya spishi,'' anaongeza Dk. Kalashnikova.
Nyangumi huyo dume aliyehama alikuwamo katika kundi la nyangumi wenye nundu ambao walinaswa katika picha iliyochukuliwa kutoka kwenye meli ya utafiti pwani ya bahari ya pasifiki nchini Colombia mwaka 2013.
Katika jambo la kushangaza alionekana tena kwenye pwani hiyo mwaka 2017 na baadaye 2022 alikutwa Tanzania kisiwani Zanzibar.
Uhamaji huo wa umbali wa kilomita 13,046, haionekani kuwa ni kawaida ambao nyangumi huyo angeweza kuchukua, lakini wanasayansi wanasisitiza kuwa bado ni mrefu zaidi kuwahi kurekodiwa.
Wanasayansi wanaeleza kwamba dunia ni duara, hivyo njia fupi ni kati ya maeneo mawili kwa umbali wa mzunguko mkubwa ambao ni sehemu inayounganisha sehemu mbili kwenye duara dunia.
Matokeo ya utafiti huo yamejumuisha maelfu ya picha za nyangumi zilizowasilishwa na watafiti, waangalizi wa nyangumi na wanajamii katika tovuti ya sayansi ya happywhale.com.
Hifadhi hiyo ambayo hutumia akili mnemba kulinganisha maumbo na mifumo ya mapambo ya mkia wa nyangumi mwenye nundu na hivyo kuorodhesha harakati zao duniani kote.
Nyangumi kuonekana katika bahari ya Tanzania siyo jambo geni, bali inaelezwa kila mwaka kuanzia mwishoni mwa Julai, wanyama hao hufika hifadhi ya bahari iliyoko Mtwara kwa makundi kwa makundi wakitokea Bahari ya Kusini.
Katika kipindi hicho nyangumi kutika nchi za Afrika Kusini na Msumbiji, hukaa kwenye hifadhi hiyo mpaka mwezi Novemba.
Wanyama hao huwa na tabia ya kukaa kwenye maeneo tofauti tofauti kutegemeana na misimu inavyobadilika. Hata hivyo, kwenye kila ukanda wa bahari huwa na eneo maalumu ambalo hufanya makazi yao.
Inadaiwa kuwa kwa ukanda wa Bahari ya Hindi na nchi za Afrika, mashariki Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na maingilio ya Mto Ruvuma ndiyo sehemu pekee inayowavutia wanyama hao kuishi.
Paul Maige ambaye ni Mhifadhi wa Bahari na mwongoza watalii wa ghuba hiyo, anasema kuwa sababu kubwa zinazowafanya wanyama hao wavutiwe kukaa kwenye hifadhi hiyo ni kutokana na kuwa na mazingira salama na yenye joto, tofauti na maeneo wanayotoka ambayo yana baridi.
Anasema wanapofika kwenye eneo hilo hutumia muda huo kwa ajili ya kujamiana ili waweze kuzaana.
Hata hivyo, uhamaji wa nyangumi huyo ni jambo la kushangaza kwa sababu hatoki katika nchi za kusini na badala yake anatokea bara la Amerika ya Kusini.
BBC
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED