Vitambue vyanzo vya ajali ili uzikwepe

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:38 AM Dec 17 2024

Ajali zinaweza kuepukwa na kuzuiliwa kwa kuwa makini zaidi.
Picha: Mtandao
Ajali zinaweza kuepukwa na kuzuiliwa kwa kuwa makini zaidi.

UMOJA wa Mataifa (UN), unazitaja ajali za barabarani kuwa ndizo zinazoongoza kuua vijana Afrika.

Ni tangazo la Mei mwaka jana, linalozitaja serikali za Afrika zichukue hatua mpya za pamoja kuzikabili, taarifa hizi zinawafikia wananchi wakati wa Wiki ya Kimataifa ya Usalama Barabarani, inayoadhimishwa Mei 15 hadi 21kila mwaka.

Ajali ni kitisho cha maisha kwa Watanzania mfano mabasi ya A-N Classic likitokea Mbeya kwenda Tabora liliua 12 na kujeruhi zaidi ya 30 wakati Asante Rabi lililosababisha vifo vya watu wanane na kujeruhi 39 mkoani Mwanza.

Kutokana na ajali hasa kuelekea wakati huu mwisho wa mwaka ni lazima kila mmoja kujilinda, kujiepusha na kusaidia wanaopata ajali. 

Ajali au dharura zinaweza kusababisha majeraha na maumivu, ulemavu, vifo na uharibifu wa mali na hivyo kuleta umaskini kwa watu na taifa.

Ili kuziepuka ni vyema kukumbushana suala la kutii sheria za usalama barabarani maana ndiyo mwongozo.

La kwanza madereva kumbukeni upande unaotakiwa kukaa wakati wa kuendeshea. Angalia wakati gani taa zinaruhusu au kukataza kuvuka na kuheshimu maelekezo.

Mambo yasiishe hapo ni vyema kukumbuka kuheshimu vivuko vya watembea na kuwajali wenye ulemavu, watoto wadogo na wazee.

Jingine ni kuacha kuendesha magari mabovu, kuepuka kuendesha gari ukiwa umelewa na kama umepanga kunywa kodi gari au omba dereva mwingine wa kukuendesha.

Acha kuendesha gari kwa kasi wala kwa mwendo mdogo fuata maelekezo ya kasi ‘speed’ yanayoonyeshwa kwenye barabara.

Jambo muhimu ni kufunga mkanda kila wakati unapokuwa kwenye gari.

Ni jambo la kuzingatia, kadhalika mlinde mtoto kwenye kiti chake na kumfunga mkanda.

Kama unaendesha pikipiki vaa kofia ngumu dereva na abiria wake. Aidha ni vyema kuzima simu na usiendeshe gari au pikipiki ukiwa unachati, unatuma ujumbe au kusikiliza muziki ukiwa na foni masikioni.

Uoni hafifu ni kisababishi cha ajali kwa hivyo kwa kuzingatia jukumu la dereva kuepusha hatari pima macho kila unapohitaji leseni au kila wakati kuhakikisha uzima wake kwa kuwa wewe ni dereva.

KUSAIDIA MAJERUHI

Kwa ujumla ajali zipo na pengine haziepukiki ili kusaidia majeruhi ni muhimu na cha kwanza kuangalia ni uhai wa mtu unayemwokoa pamoja na uzima wako.

Hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari usigusane na damu za majeruhi kuepusha kuambukizwa maradhi.

Kingine muhimu ni kujua kuwa majeruhi hufariki kutokana na kutokwa na damu nyingi pamoja na kukosa hewa safi baada ya kubanwa au kuumizwa mfumo wa hewa.

Ikumbukwe kuwa ubongo wa binadamu hauwezi kuishi bila hewa safi ya oksjeni kwa dakika sita baada ya hapo hufa.

Kwa hiyo kwa majeruhi yeyote ni lazima mfumo wa hewa ufuatiliwe na hasa namna ya kupumua kama inavyopasa na pia kumhakikishia mzunguko wa damu na kufahamu iwapo anajitambua au amepoteza fahamu.

Kikubwa kingine cha kuwaangalia majeraha ni iwapo njia ya hewa iko salama na mgonjwa anapumua na kama kuna sehemu inayotoka damu izuie.

Watu wasiwasonge na kuwazingira majeruhi, kaa mbali wapate hewa, fungua vifungo, tai, mikanda na kulegeza nguo zinazowabana.

Acheni kuwaibia majeruhi au kuwaia ili kupora mali. Ni jinai.

KUZUIA AJALI

Anza na epusha kunguka. Watoto ni kundi linaweza kuanguka chini wakati wote. Ni vyema wawe na waangalizi muda wote nyumbani na popote.

Kadhalika waangaliwe hata wakati wanapocheza wawe salama na vifaa wanavyotumia viwe salama pia.

Kama ni ndani ya nyumba waangaliwe wasicheze kwenye sakafu yenye maji watateleza. Kuwe na mwanga wa kutosha.

Wasioona wawe na waangalizi. 

KUACHA UGOMVI  

Mambo yanayosababisha ugomvi ni mengi lakini mojawapo ni ulevi epuka. Achana na kutumia dawa za kulevya, pombe na bangi kwani vinachangia ugomvi.

Lakini pia si vyema kujichukulia maamuzi ya kuwaadhibu wengine, watu waaache kujichukulia sheria mkononi kwa kuwaadhibu watuhumiwa wa makosa mbalimbali.

HADHARI YA MOTO

Moto unaweza kusababisha hatari  hivyo watoto wasiachwe bila uangalizi kwani ni rahisi kuangukia maji yanayochemka, vyakula hasa chai au uji na moto wenyewe.

Kwa wenye kifafa, wagonjwa na wazee ni lazima waepushwe na ajali na kuwapa wasaidizi tena wasikae karibu na moto na maji ya moto.

Wakati mwingine umeme nao ni chanzo cha ajali watu wajali na kuzingatia masuala ya usalama na kutumia vifaa vya umeme kwa usahihi.

Mfano, ukimaliza kupasi ichomoe kwenye moto, kuzuia ajali kwenye mifumo ya nyumbani.

Ulevi kupindukia ni jambo linaloweza kusababisha ajali ya moto, mfano kuwasha jiko ili kupasha chakula au kupika kisha kujisahau, kuwasha pasi na kujisahau, kuwasha sigara na kujisahau na kusababisha kuchoma godoro chumba, meza na viti sebuleni.

UANGALIFU MAJINI

Ajali hizi zinaepukwa kama huna ujuzi wa usalama wa maji usiingie majini. Kadhalika kama unakwenda ufukweni na watoto wasimamie wakati wote.Wafuatilie na weke jicho lako kwa watoto wanapokuwa ndani au karibu na maji. Usiruke ndani ya maji ili kuokoa mtu utazama kama huna uwezo. Ni vizuri kuweka uzio kuzunguka bwawa la kuogelea kunusuru watoto.Kama umelewa acha kuogelea na pia mvua zinanyesha umelewa na unataka kuvuka mto au mkondo acha unaweza kuzama.Aidha ukiwa na akili timamu ingiza fimbo kupima kina cha maji na si miguu, lakini kama kuna mvua kubwa na mafuriko usivuke mto na ikibidi kaa mbali na mifereji ya maji, mito na madimbwi.

EPUKA WANYAMA

Zipo ajali zinazoweza kutokea kutokana na wanyama mfano kwa wanaoishi vijijini au waliozungukwa na vichaka ni vyema kuwa waangalifu na wanyama kama nyoka na hata simba au chui.

Kwa wanaoogelea ni vyema pia kujikinga na mamba mtoni. Kumbuka kuepuka kuingia vichakani wakati wa jua, kadhalika kutembea peke yako nyakati za usiku.