Zama za Dk. Samia na Ujamaa katika uchumi – siasa zinavyosafiri nchini

By Peter Orwa , Nipashe
Published at 08:20 AM Dec 13 2024
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Picha:Mtandao
Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

KATIKA uchambuzi wa ukurasa wa 12, ulikuwa na mustakabali mpana wa tafsiri na nafasi ya Ujamaa, ndani ya mabadiliko ya kihistoria, Tanzania inapitia. Je swali linabaki, katika uongozi wa Awamu ya Sita, nini nafasi ya Ujamaa? Pata ufafanuzi wa mwandishi PETER ORWA.

WAKATI mikakati ya kiuchumi ikiendelea nchini, unapoingizwa muktadha wa ama mwenendo  wa kiserikali unaendeshwa na siasa za Ujamaa, au sivyo ni zao lenye jibu kwa ‘hoja kwa vielelezo.” 

Kikubwa cha uzoefu ni katika Awamu Tatu za uongozi kiserikali nchini, hasa kuanzia zama za uongozi wa marais Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na John Magufuli, kuna nyendo za Kijamaa zimetumika, ndani ya mustakabli wa mfumo huria. 

Mosi, uhalisia unaanzia katika Katiba ya Nchi (inayojadiliwa) inagusa kutambua matumizi ya nyendo hizo, pia Sera ya Elimu iliyopo ya mwaka 2014, inatumia ‘Elimu ya Kujitegemea’ ambayo ni zao la Azimio la Arusha, ikiwa na maana ya Ujamaa katika tafsiri yake “Njia Pekee ya Kujenga Jamii ya Watu Walio Sawa na Huru.” 

Hadi sasa uongozi wa Rais Dk. Samia, unadumu nayo Elimu ya Kujitegemea, ambayo inabeba maudhui makuu kadhaa yaliyobuniwa na Rais na Mwenyekiti wa chama tawala – TANU mwaka 1967. 

Mosi, ilitaka elimu ya kitanzania kurejea maudhui ya maisha ya utanzania; kila anayepata elimu hiyo akanufaishe umma wake; kila ngazi ya elimu ijitosheleze na kuweza kutumika.  

Hapo ikamaanisha ngazi anayohitimu shule ya kitanzania, iweze kutumika kwa ufanisi na si mhusika kuhesabika hajafaulu na ndio maana walioshindwa mitihani darasa la saba, walitafsiriwa ‘hawajaendelea’ na siyo ‘kufeli’, huku walioshinda mtihani ‘wamechaguliwa kujiunga sekondari.’

 Bado ambao hawakuchaguliwa walitarajiwa elimu yao kuwafaa katika shughuli zao kimaisha mfano shambani. Hiyo ni sababu mojawapo katika shule za sekondari kuanzishwa mikondo; Biashara, Ufundi, na Sayansi. 

Wakati katika mfumo wa kiuchumi ukiwa hivyo, serikali inazama zaidi katika mrengo wa kulia kuzalisha, serikali ikibaki mratibu mkuu na kukaribisha uwekezaji, mathalan kasi inayoendelea kukaribisha viwanda vya mbolea nchini. 

Pia, hatua kama hiyo ndio iko katika kukodisha uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam. 

Hata hivyo, serikali katika upande wa pili wa shilingi, ikawajibika moja kwa moja katika kuziba mapengo ya shida za kijamii zinazojitokeza, hasa pale nyenzo binafsi zinapokwama. 

Hapo ni katika maeneo kama viwanda vya sukari, vilivyo chini ya mifuko ya uwekezaji kukabili uhaba wa sukari kitaifa, vivyo hivyo kwa kuanzisha kiwanda cha viuatilifu. 

Ni dhana inayoenda mbali katika mustakabali wa elimu, pale yalipoonekana mapengo katika fursa za kielimu na kiafya, serikali imeingilia moja kwa moja. 

Kuanzia na safari ya kihistoria, pengo la elimu ya sekondari kuanza kuzibwa kiserikali kupitia kubuniwa sekondari za kata katika awamu ya tatu ya uongozi, ikaenda mbali kuboreshwa kimahitaji katika awamu ya nne. 

Inapotajwa, uongozi wa awamu ya tano Rais Dk. Samia akiwa Makamu wa Rais, ulibaini ada ya Sh. 20,000 kwa sekondari ulikwamisha baadhi wazazi kupeleka watoto shule, hata ikafutwa rasmi hadi kidato cha nne. 

Lakini hilo likaonekana kuwa ni tatizo bado na ilipongia serikali ya awamu ya sita, ikafuta hadi kidato cha sita, kwa ujumla wake ukaongeza ujio wa wanafunzi wapya maradufu, sambamba na shinikizo la kisheria, hata wakamiminika wanafunzi wengi wakiwamo kutoka jamii za wafugaji.

 Hatua kama hiyo, ikafanyika hata katika ngazi ya elimu ya juu, iwe haki ya kila mtoto wa Kitanzania, hasa pale katika Awamu ya Sita ya uongozi wa nchi, Rais Dk. Samia akatangaza kupanuliwa  fursa na haki za wanafunzi wa elimu ya juu kupata mikopo ya elimu, si ngazi ya vyuo vikuu pekee, bali hata wa chini yao wanaosomea diploma. 

Pia, Rais katika awamu iliyoko sasa, akawaandalia wahitimu urahisi kwamba, mikopo hiyo sasa itarejeshwa bila ya riba na kuwa  haki ya kila mwanafunzi na si makundi fulani pekee. 

Hapo ikirejewa tafsiri hiyo kisiasa, ni utekelezaji wa nguzo ya kijamaa ndani ya mfumo wa uchumi huria, kama ambao unatumiwa na vyama vya Labour Uingereza na Democrat, Marekani.

 Kuna marejeo hapo ya mgombea Barack Obama wa Marekani, alitumia shida ya watu wa chini katika afya, kuanzisha bima ya afya rahisi kwa wengi na ikamvusha kisiasa  

NAFASI JINSIA

Eneo lingine la tafsiri ya Ujamaa huria, ni pale Rais Dk. Samia akawekeza jinsia yake kunadi hali za wanawake wanaokwazwa katika mengi kisiasa. 

Kurejea katika fursa za elimu ya juu, ikiwamo kuwa na mifuko ya kusomesha mabinti hata inawawezesha kitaaluma, ambayo zao lake inawang’arisha mbele kimaisha. 

Pia, kwa kutumia Mpango wa Maendeleo ya Msingi (MMAM) ameboresha huduma za vituo kwa ujenzi na upanuzi wa vyuo vingi sana vya afya kitaifa, ambayo katika hali halisi umma, ndio unamudu kuliko binafsi. 

Sura hiyo ndio kuna kundi kubwa la kinamama wanaopewa fursa za kiutendaji katika uongozi, ikionekana wazi sasa kuanzia ngazi ya chini hadi Baraza la Mawaziri. 

Mtazamo wa wote, unarejesha katika majumuisho ya nadharia za kijamaa, pale kunapokuwapo mapengo ya kijamii, hasa katika kundi la waliokosa kufanyiwa upendeleo wa kisiasa wanufaike.