Funguo,msako madalali ufanikishe NHC mpya

Nipashe
Published at 07:39 AM Jul 02 2024
news
Picha: Mtandao
Nyumba mradi wa Samia Kawe.

MADALALI wa nyumba za Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), waliokuwa wakitamba mjini kwa kuwapangisha wengine kwa gharama kubwa na kujinufaisha, arobaini zao zimetimia.

Ni baada ya serikali kuliagiza shirika hilo kufanya  operesheni ya kuwaondoa watu wanaofanya udalali na kwa na sasa NHC inaandaa mikakati ya msako huo nchi nzima.

Ni hatua mahususi ya kuwezesha  nyumba hizo kubakia kuwa mali ya umma na zisiendelee kugeuzwa kuwa vitega uchumi na miradi ya watu wachache wanaojinufaisha tena kwa fedha nyingi.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geoffrey Pinda, ndiye anayetoa maelekezo  na kuagiza hatua hiyo ichukuliwe  baada ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, kutembelea miradi ya shirika hilo jijini Dar es Salaam.

NHC imekuwa moja ya eneo ambalo watu wanajinufaisha hasa kutokana na uhitaji wa makazi  bora na kwa gharama nafuu. 

Ni wazi kuwa kuna wakati shirika hilo lilitangaza kuwa lingetoa ufunguo wa kielektroniki kama ‘LUKU’ ambao kama mteja hajalipa kodi mlango ungejifunga, yote hayo yakilenga kuzuia kuchelwesha malipo.

Ni wazi kuwa hatua ya kutoa ufunguo ingeendana na kuwatambua wapangaji halali na kuwatambua kwa vitambulisho halali kama vya taifa, pasi  za kusafiria na alama za vidole hata hivyo bado hakuna kilichosikika kuhusu mkakati huo, ambao NHC wanafahamu kinachoendelea.

Ni wazi kuwa kuna haja ya kuliendesha shirika  hilo kwa ubunifu na hata kielektroniki lakini si nyumba za NHC tu pengine hata za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) , ambazo nazo kuna madai kuwa kuna  wajanja wanazifaidi. 

Kama anavyowakumbusha  Naibu Waziri, serikali inataka wapangaji wa nyumba hizo wajulikane ili waweze kupewa upangaji rasmi badala ya kuwa wanalipa fedha nyingi kwa watu ambao hawahusiki na nyumba hizo.

Tunaona hatua hiyo ni muhimu na itasaidia kuwapunguzia gharama kubwa ambazo baadhi ya wapangaji wa nyumba hizo walikuwa wanakumbana nazo kutokana na ujanja unaofanywa na watu wachache.

Kwani kwa mujibu wa Naibu Waziri, serikali inafahamu  kuwa watu  wanachukua fedha nyingi kwa kupangisha wengine, jambo  ambalo ni wazi wapangaji wanaumia lakini  wajanja wakinufaika.

Ni wazi  kitendo cha baadhi ya watu kuchukua nyumba zaidi ya 10 na kupangisha wananchi kwa gharama kubwa ni sawa na kuwaumiza na kufanya wengine kuziona nyumba hizo kama ni mali binafsi au zinazoendeshwa kijanja licha ya kuwa ni mali ya umma.

Lakini pia tunadhani kitendo hicho kinaweza kusababisha wapangaji kushindwa kulipa pango kwa wakati kwa NHC lakini wakiwanufaisha matapeli kutokana na ukweli kwamba wanawahofia madalali kuliko mmiliki halali.

Ni miongoni mwa mambo yanayolisababishia shirika hasara au hata kushindwa kukamilisha miradi yake kwa wakati kutokana na ukosefu wa fedha zinazotoka kwa wapangaji wake.

Hivyo, uamuzi wa kuwaondoa wanaofanya udalali wa nyumba za NHC ni hatua bora ambayo pengine ilichelewa . 

Ni vyema pia NSSF ikaliangalia hilo na kuchukua hatua kama ambavyo shirika la nyumba limefanya ili kujihakikishia mapato yanayovuja kwa njia kama hizo za madalali. 

Tunaamini kwamba msako huo ukifanyika kikamilifu, utakuja na matokeo chanya ambayo yatasaidia shirika kuwa na wapangaji sahihi watakaolipa kodi na kuchangia kuendeleza na  kuimarisha NHC kimapato.

Hatuna maana kwamba waliomo sio sahihi, bali inawezekana walipatikana katika mazingira hayo ya udalali na kufanya fedha nyingi kuishia kwa madalali, huku shirika likipata kidogo.

Kwa maelekezo hayo ya serikali kutaka shirika lianzishe msako, tunaona kuwa inawezekana ikawa suluhisho la kudumu ili NHC ipate  wapangaji halali watakaolipa kodi kwa wakati.

Lakini pia, iwe ni fursa kwa watu wenye kipato cha kawaida kutumia nyumba hizo badala ya kuziona kuwa ni za watu wa tabaka la juu kwa maana ya wenye kipato kikubwa.