Ajabu kuchangamkia fursa kwenye maafa

By Moshi Lusonzo , Nipashe
Published at 10:04 AM Nov 20 2024
Ajabu kuchangamkia fursa kwenye maafa
Picha: Mtandao
Ajabu kuchangamkia fursa kwenye maafa

JUMAMOSI ya Novemba 16, Watanzania walianza siku kwa majonzi na hofu, baada ya jengo la ghorofa nne kuporomoka Kariakoo jijini Dar es Salaam na kuua watu 16 kwa taarifa za juzi jioni.

Jengo hilo limesababisha idadi kubwa ya watu kunaswa kwenye vifusi na bado kazi ya uokoaji inaendelea.

Kwa muda wa siku tano juhudi za kuwasaka manusura  zinafanyika mchana na usiku  huku serikali ikithibitisha vifo vya watu 16 na wengine 86 wamejeruhiwa na kupelekwa katika hospitali mbalimbali kutibiwa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wakati akiongoza wananchi  kuwaaga  waliofariki  katika tukio hilo, alionesha kusikitishwa na baadhi ya watu kuchukulia majanga hayo ya kitaifa kama mtaji wa kujipatia fedha kwa kuwachangisha watu fedha za kusaidia walioathirika.

Katika kuonesha hapendezwi na tabia hiyo, Waziri Mkuu, analitaka Jeshi la Polisi kumkamata Jennifer Jovin, maarufu kama Niffer, baada ya kuchangisha fedha kutoka kwa wananchi kwa madai ya kusaidia waathirika wa tukio hilo.

Pamoja na kutoa agizo hilo, alipiga marufuku kwa yeyote kuchangisha fedha katika matukio ya maafa, akieleza kazi hiyo inafanywa na serikali kupitia akaunti maalum inayosimiwa na kitengo cha maafa kilichoko chini ya ofisi yake.

Baada ya kauli hiyo, Jeshi la polisi lilitoa taarifa ya kumkamata mtuhumiwa huyo, huku Jennifer mwenyewe akikiri kufanya kitendo hicho na kujitetea kuwa alifanya hivyo kwa nia njema na kwamba hakujua miongozo sahihi ya uchangishaji katika matukio ya maafa.

Hata hivyo, jambo linalowafanya Watanzania kupata tabasamu ni kuona serikali imeliona tatizo hilo ambalo limekuwa na pia  kuonekana kero ndani ya jamii.

Maafa mengi yaliyotokea nyuma kama maporomoko ya Hanang, kuna baadhi ya watu na taasisi mbalimbali walichangisha fedha nyingi, lakini haikujulikana kama kweli ziliwasilishwa katika sehemu sahihi au ziliishia kwenye mikono na matumbo ya watu.

Ilikuwa jambo la kawaida kuona watu na taasisi hizo zikitangaza michango katika kurasa zao za mitandao ya kijamii au katika vyombo vya habari zikieleza kutaka kwenda kusaidia jamii zilizoathirika.

Hata hivyo, pamoja na kujipatia fedha nyingi za michango, hakuna mrejesho wa matumizi au uwasilishaji wake sehemu zilizotakiwa kwenda.

Kwa maana nyingine, hakuna aliyejua fedha hizo zimekwenda wapi, licha ya Watanzania wengi wenye tabia ya upendo na kujitoa kujitokeza kuchangia.

Waziri Mkuu kupiga marufuku uchangishaji fedha katika matukio hayo yanayogusa hisia za watu, ni sawa na kuweka asali kwenye kidonda kibichi kwani wengi walikuwa wakiumia ndani ya mioyo yao kutokana na kushindwa mahali pa kusemea.

Wachangishaji wengi ni watu wenye nguvu na wapo karibu na viongozi wa serikali, hivyo pengine jamii haikuona wakiguswa wala kuulizwa. Wengi wakaamini kuwa ni  kwa kuhofia kuonekana kuwa kufanya hivyo sio uzalendo.

Si katika matukio ya maafa tu ambayo wananchi tunapigwa, hata katika misiba au ugonjwa kwa watu mashuhuri tumesikia malalamiko ya watu wanajiweka mbele kwa kusimamia michango na kisha kutoweka nayo.

Hiyo ndio jamii tunayokuwa nayo kwa sasa ambayo kimsingi imekuwa haina hofu ya Mungu na imejaa ubinafsi na kusaka mali kwa hali yoyote.

Waziri Mkuu  kuliona hilo na kukemea hadharani, ni sawa na kutoa mwanga kwamba tunapoelekea sawa tunakwenda shimoni, hivyo tubadilike na kuuweka Utanzania mbele.

Wakati wa kurudi kule tulipotoka umewadia, kwani wenzetu wakipata matatizo tujitokeze kuwafariji badala ya kugeuza kuwa mtaji wa kujikusanyia fedha.

Tusisubiri tena kiongozi wa juu ajitokeze kukemea mambo kama haya, sisi wenyewe tunaweza kukomesha kwa kuacha kujitokeza kuchangia michango ambayo hatuna uhakika nayo kama inalenga kusaidia au kwenda kwenye mifuko ya watu ambao hawana utu.