RAS ahimiza wajasiriamali kufikiwa, wakuze mauzo

By Christina Haule , Nipashe Jumapili
Published at 04:59 PM Aug 10 2025
Wajasiriamali watakiwa kuona umuhimu wa kupata nembo
Picha: Christina Haule
Wajasiriamali watakiwa kuona umuhimu wa kupata nembo

KATIBU Tawala Mkoa wa Morogoro, Musa Musa, amewaomba Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kuhakikisha linawafikia wajasiriamali, ili waone umuhimu wa kupata nembo na kufanikisha mauzo ya bidhaa zao.

Musa amesema hayo wakati akizungumza na wajasiriamali kwenye viwanja vya maonesho ya kilimo, Nanenane, Kanda ya Mashariki, yanayofanyika mkoani Morogoro.

Mmoja wa wajasiriamali hao, Felister Milinga, amesema ni vema serikali ya mkoa ikaliangalia suala la wao kukosa nembo ya TBS muda mrefu na kuona na namna ya kulegeza vipengele vilivyopo.

Anasema wakiwa wajasiriamali wanaozalisha mafuta ya kukuza nywele wamekuwa wakiaminika na wateja walikwishatumia bidhaa zao huku wengine wakiingiwa hofu kwa madai ya kukosa TBS.

Mmoja wa wajasiriamali hao akiwva kwenye maonesho hayo, amesema changamoto kubwa inayowafanya kukosa nembo ya ubora ni kuwepo kwa vigezo 11 vya msingi ambavyo wakiwa wajasiriamali wadogo wanashindwa kuvitimiza vyote. 

Hivyo ameliomba Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Morogoro, kuwaweka kwenye kundi moja katika uzalishaji wa bidhaa zao, ili wafikie vigezo 11 vilivyopo na kupata nembo ya ubora (TBS).

Meneja wa TBS Mkoa wa Morogoro, Joan Nangawe, amewahimiza wajasiriamali kufika ofisi za SIDO, ili kupata maelekezo ya namna ya kupata nembo za TBS, ambazo hutolewa.