Waomba udhibiti wanunuzi holela wa mazao

By Renatha Msungu , Nipashe Jumapili
Published at 05:10 PM Aug 03 2025
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dk. Fatma Mganga, akizungumza na maofisa wa COPRA, wakati akitembelea mabanda kwenye maonesho ya kimataifa ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma
Picha: Renatha Msungu
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dk. Fatma Mganga, akizungumza na maofisa wa COPRA, wakati akitembelea mabanda kwenye maonesho ya kimataifa ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma

KATIBU Tawala wa Mkoa wa Singida, Fatma Mganga, ameiomba Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao mchanganyiko (COPRA), kuweka kambi mkoani humo, ili kuwabaini wanunuzi wakubwa wa mazao ya chakula na biashara wanaokwepa kutumia mfumo wa ununuzi.

Mfumo huo ni wa stakabadhi ghalani na ule wa minada ya kidigitali badala yake huingia shambani kwa wakulima.

Fatma amesema hayo jana jijini Dodoma, alipotembelea mabanda mbalimbali katika maonesho ya Kimataifa ya Wakulima Nanenane, yanayoendelea katika viwanja vya Nzuguni, vilivyopo mkoani hapa.

“COPRA inapaswa kuwatafuta watu hao kukaa nao pamoja kuzungumza, ili kuondoa kero ya kuviziana kwenye ununuzi, ifikapo msimu wa mavuno katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Amesema mkoani humo kumekuwa na changamoto kubwa ya ununuzi wa mazao mbalimbali kiholela na wanunuzi wakubwa, ambao hawapendi kununua mazao ya wakulima kupitia mifumo husika badala yake wao huenda kinyemela kwa wakulima mashambani.

"Hilo limekuwa tatizo kubwa sana mkoani Singida mwaka jana tumeuza kwa shida sana zao la dengu ilikuwa mvutano na wanunuzi wakubwa ambao ukimbilia kununua shambani badala ya kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani," amesema.

Aidha amesema COPRA inapaswa kurejea mkoani Singida kwa ajili ya kuwatafuta watu hao, ili wakae nao chini na kubaini kitu gani kinawafanya waende wapende kununua mazao kinyemela badala ya kutumia mfumo uliowekwa na serikali," amesema.

Ofisa kutoka COPRA, Abbas Kombo amesema hivi sasa mamlaka hiyo imedhibiti madalali wanaotumika kupeleka wanunuzi mashambani, kwa ajili ya kununua mazao.