KUNDI la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda, limekashifu vikosi vya SADC vinavyohudumu katika eneo la Kivu Kaskazini, kwa kukiuka mkataba wa makubaliaono uliopo kwa sasa.
Limesema, badala yake kushirikiana na jeshi la FARDC na makundi ya wapiganaji kama vile Wazalendo kutekeleza mashambulizi katika maeneo kadhaa ya mji mkuu wa Goma.
Kupitia taarifa walioichapisha mapema Jumapili leo, Aprili 13, 2025, M23 wanaoshirkiana na washikadau wengine kwenye muungano wa Congo River Alliance, wameeleza kero zao, kutokana na kile wamekitaja kuwa hatua zinazohatarisha maisha ya raia katika mji huo wa Goma.
“Juhudi za hivi punde zinazotekelezwa na serikali ya Kinshasa kudhibiti mji wa Goma, zimezuiwa vikali. Tumechukizwa na mashambulizi ya Aprili 11, 2025, ambayo yanatishia moja kwa moja, hali ya usalama wa raia katika eneo hilo,” amesema msemaji wa kundi hilo Lawrence Kanyuka.
Aidha, M23 sasa inasema italazimika kuchukuwa hatua na kujibu mashambulizi dhidi yao, ikiwa itaendelea kuchokozwa.
“Tutabatilisha msimamo wetu wa awali, ikiwa mambo yataendelea kuwa hivi. Jukumu letu kuu ni kuhakikisha kwamba maisha na mali ya raia wa Congo imelindwa.” Amesema bwana Kanyuka katika taarifa hiyo ya Jumapili.
Kundi hilo limesisitiza kwamba liko tayari kuhakikisha kwamba maisha ya raia yanalindwa katika eneo zima la mashariki mwa DRC na hawatosita kuchukua hatua wanazohisi zinafaa kufanya hivyo.
Kundi hilo ambalo lilitarajiwa kutuma ujumbe wake nchini Qatar wiki jana kwa mazungumzo ya moja kwa moja na upande wa serikali, limesalia kimya kuhusu hatua iliyopigwa katika juhudi hiyo ya kutafuta amani.
Awali, M23 walikuwa wametoa masharti ambayo waliyataka kuangaziwa kama jambo muhimu kabla ya kushiriki kwenye mazungumzo yoyote. Walilalmikia vikwazo vilivyowekwa dhidi ya viongozi wake wakuu kwa pamoja na maofisa wakuu katika jeshi la Rwanda.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED