Dk.Batilda Buriani: Tanga inajitosheleza kwa chakula

By Hamida Kamchalla , Nipashe Jumapili
Published at 12:20 PM Oct 12 2025
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi, Dk. Batilda Buriani
PICHA:HAMIDA KAMCHALLA
Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi, Dk. Batilda Buriani

MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi, Dk. Batilda Buriani amesema serikali ya awamu ya sita imefanikiwa kuhakikisha uzalishaji wa chakula nchini unaimarika na kutosheleza mahitaji ya nchi kwa kipindi chote.

Hayo ameyasema leo wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya chakula duniani yanayofanyuka Kitaifa mkoani humo katika viwanja vya shule ya sekondari Usagara, jijini Tanga.

Dk. Buriani amesema hali ya uzalishaji na upatikanaji wa chakula katika Mkoa wa Tanga inatosheleza ambapo katika msimu wa kilimo mwaka 2024/25 chakula chake kinatumika mwaka 2025/26, ambapo jumla ya hekta 102,076 zililimwa  na kuzalisha tani 1,814,285.2.

"Kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Tanga ulikuwa na watu 2,615,597 ambao mahitaji yao ya chakula ni tani 621,025, hivyo kufanya Mkoa kuwa na ziada ya chakula" amesema mkuu huyo.

Amesema Mkoa umeendelea kusimamia mpango wa serikali wa kuimarisha tija na uzalishaji wa mazao makubwa ya kimkakati ambayo ni mkonge, korosho, kahawa, pamba, chai na alizeti ambayo ni muhimu kwa mkulima kujipatia kipato.

"Pamoja na hali nzuri ya uzalishaji wa vyakula, bado watu wetu wanakabiliwa na tatizo la lishe duni, hali inayosababisha matatizo ya kiafya hususani kwa watoto wadogo chini ya umri wa miaka mitano, hata hivyo Mkoa umeendelea kufanya juhudi mbalimbali kukabiliana na tatizo hili" amesema.