Wanne mbaroni tuhuma mauaji mtumishi TRA

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 09:26 AM Dec 08 2024
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro.

SIKU mbili baada ya watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kujeruhiwa kwa kipigo kutoka kwa wananchi na mmoja kuripotiwa kufariki dunia, Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, limetangaza kuwashikilia watu wanne kwa tuhuma za mauaji.

Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Jumanne Muliro, aliwataja wanaowashikilia ni Deogratius Massawe (49) na Iddi Bakari (30), wote wakazi wa Tegeta kwa Ndevu, wote makuli.

Wengine aliwataja ni Omar Issa (47) ambaye ni mpiga debe wa bodaboda, mkazi wa Bunju, Kinondoni, Dar es Salaam na Rashid Mtonga, (29) dereva wa bodaboda mkazi wa Bunju, Dar es Salaam.

Kamanda Muliro alisema wanatuhumiwa kufanya mauaji ya mtumishi TRA, Amani Simbayao na  kumjeruhi Adriano Fredrick.

“Watuhumiwa hao na wengine ambao bado wanahojiwa kwa kina, walikamatwa baada ya kuwashambulia maofisa hao wa TRA wakati wakitekeleza majukumu yao ya kisheria.

“Waliliharibu pia, gari namba STL 9923 aina ya Toyota Land Cruiser Hardtop jeupe mali ya TRA. Tukio lilitokea Desemba 5, mwaka huu, saa 3 :00 usiku, Tegeta kwa Ndevu, Kinondoni, baada ya maofisa hao wa  TRA kukamata gari namba T 529 DHZ aina ya BMW rangi nyeupe lililodaiwa kuwa na makosa ya kikodi,” alisema.

Kamanda Muliro alisema Jeshi la Polisi linaonya vikali na kwamba halitavumilia watu ambao wanataka kujenga tabia ya kuwashambulia watumishi wa serikali wakati wakitekeleza majukumu yao, licha ya kuwa wanakuwa wamefuata taratibu zote za kisheria.

Alisema jeshi halitasita kuchukua hatua kali za haraka na za kisheria dhidi ya wahusika kwa kuwafikisha kwenye mamlaka zingine za haki.

Taarifa  iliyotolewa juzi usiku na TRA, iliutangazia umma kwamba mfanyakazi wake, Simbayao, amefariki dunia juzi mchana akiendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

“Bodi ya Wakurugenzi, Menejimenti na Watumishi wa TRA inasikitika na kutoa pole kwa familia, ndugu na jamaa, kutokana na kifo cha mtumishi wetu wa TRA Amani Simbayao.

“Kifo hicho kilitokea juzi (Desemba 6) mchana  Hospitali ya Muhimbili alikolazwa baada ya tukio la shambulio akiwa katika majukumu yake ya kiazi kwa maslahi ya taifa eneo la Tegeta kwa Ndevu,” ilisema taarifa hiyo.

Watumishi hao wanadaiwa kushambuliwa na wananchi wakati wanatimiza wajibu wao wakihusishwa na kitendo cha utekaji, kilichosababisha wao na gari kushambuliwa.

Gari lililokuwa likifuatiliwa ni namba T 229 DHZ aina ya BMW X6 linalodaiwa kuingizwa nchini kinyume bila kulipa kodi za serikali stahiki kwa mujibu wa sheria, hivyo watumishi hao walikuwa wakiifuatilia kwa lengo la kuikamata, ili kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za kodi.