MAKAMU wa Rais wa Dk. Philip Mpango, amesema marehemu Dk. Faustine Ndugulile, Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, alikuwa kiongozi mwenye nidhamu, rafiki wa kila mtu na kiongozi aliyetetea vyema maslahi ya taifa.
Dk. Ndugulile ambaye ni Mbunge wa Kigamboni, Dar es Salaam, alifariki dunia Jumatano ya wiki hii wakati akiendelea na matibabu nchini India kwa maradhi yaliyokuwa yanamkabili na mwili wake kuwasili Tanzania juzi.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu Kigamboni alikoenda kwa ajili ya kuifariji familia yake, Dk. Mpango amewaombea faraja na moyo wa uvumilivu walioguswa na msiba huo.
Aliwashukuru wote walioshiriki katika kuifariji familia hiyo katika kipindi kigumu kwao na kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kushirikiana katika nyakati mbalimbali zinazojitokeza katika jamii ikiwamo za majonzi na furaha.
Dk. Mpango alisema inapaswa kuendelea kumshukuru Mungu kwa maisha ya Dk. Ndugulile hapa duniani.
“Ni vema kwa Watanzania kuendelea kuishi vizuri na ndugu na majirani,” alisema.
Akiwa nyumbani hapo, Makamu wa Rais amesali pamoja na familia, ndugu, jamaa na marafiki kumuombea marehemu.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, kesho mwili utatolewa Lugalo na kupelekwa Parokia ya Mtakatifu Immaculata, Upanga, Dar es Salaam, kwa ajili ya ibada na kisha utapelekwa viwanja vya Karimjee kwa ajili ya mazishi ya kitaifa, yatakayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Baada ya Karimjee, mwili utalala nyumbani kwake Kigamboni na Jumanne, utapelekwa viwanja vya Machava, Kigamboni kwa ajili ya wananchi wake kumuaga na baadaye utazikwa katika makaburi ya Mwongozo, yaliyoko Kata ya Mwongozo, wilayani Kigamboni.
Dk. Ndugulile aliyezaliwa Machi 31, 1969, alifariki dunia Novemba 27, mwaka huu, akiwa nchini India alikokwenda kutibiwa.
Juzi, Dk. Mpango alifika pia, nyumbani kwa aliyewahi kuwa Msajili wa Hazina Marehemu Dk. Oswald Mashindano, aliyefariki dunia Jumatano ya wiki hii na kuifariji familia yake.
Akizungumza na waombolezaji, Makamu wa Rais aliyeambatana na mwenza wake, Mama Mbonimpaye Mpango, alisema marehemu Dk. Mashindano aliyezikwa jana makaburi ya Kinondoni, amefanya kazi vizuri na kwa uaminifu mkubwa enzi za uhai wake.
Alisema katika nafasi mbalimbali alizowahi kutumikia ikiwamo Msajili wa Hazina aliweza kutoa mchango mkubwa katika taifa kupitia utafiti mbalimbali alizowahi kufanya hususani za maendeleo ya kilimo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED