Inter Zanzibar kujipanga mzunguko wa pili

By Hawa Abdallah , Nipashe Jumapili
Published at 02:35 PM Dec 01 2024
  Inter Zanzibar kujipanga mzunguko wa pili.
Picha: Mtandao
Inter Zanzibar kujipanga mzunguko wa pili.

KOCHA wa Inter Zanzibar FC, Hassan Mohmed amesema licha ya kupokea vipigo mfululizo katika michezo ya Ligi Kuu ya Zanzibar, lakini bado anaimani timu hiyo itafanya vizuri katika mzunguko wa lala salama.

Inter Zanzibar imeendelea kugawa alama katika michezo ya Ligi Kuu ya Zanzibar inayoendelea Visiwani hapa, ambapo juzi Ijumaa katika michezo wao wa 14 ilifungwa mabao 4-1 na Mwenge SC kutokea Pemba.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, kocha Mohamed alisema bado wana nafasi ya kurekebisha makosa yao na kurudi tena upya kwa kufanya mipango itakayo kuwa na faida ili kupata alama za kuwabakisha Ligi kuu.

Alisema bado ni mapema kupoteza matumaini ya kubaki ligi kuu kwakuwa mipango yao ni kuhakikisha wanakifanyia maboresho makubwa kikosi chao.

“Bado tunayo nafasi ya kuibakisha timu ligi kuu kwa kujipanga upya, mzunguko wa kwanza hatukuwa vizuri,” alisema.

Inter Zanzibar sasa imefungwa michezo 11 kati ya 14 iliyocheza na imemeshinda mchezo mmoja na kutoka sare mara mbili.

Na sasa ipo nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na alama tano, wakati anayeburuza mkia ni Tekeleza FC yenye alama  tatu.