Tabora yaahidiwa milioni 200 ikimaliza tatu bora

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 02:30 PM Dec 01 2024
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha.
Picha:Mtandao
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha.

MKUU wa mkoa wa Tabora, Paul Chacha, ameipongeza timu ya Tabora United kwa kuendelea kufanya vyema kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, huku akiiahidi kuizawadia Sh. Milioni 200 iwapo itamaliza kwenye nafasi tatu za juu.

Mkuu wa mkoa huyo alisema hayo mkoani humo baada ya timu hiyo kuifunga KMC mabao 2-0, mechi iliyochezwa juzi Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, ikiwa ni mechi ya tano kwa timu hiyo kucheza bila kupoteza.

"Wao wanatakiwa wajitahidi tu, wakimaliza kwenye nafasi tatu za juu ligi itakapokuwa imeisha, yaani ligi imeisha na wapo ndani ya tatu bora, tunawawekea  Sh. Milioni 2000 mezani, zawadi yao hiyo. Wakishindwa sasa hiyo ni juu yao, lakini sisi tumeamua hivyo, ile ni timu yetu ya mkoa tunatakiwa kuilea. Walikuwa hawana basi tumewanunulia, kwa sasa hawana shida na mishahara wala posho yoyote kila kitu kiko sawa, wakishindwa kucheza mpira ni wao," alisema Mkuu wa mkoa huyo.

Aliwapongeza wachezaji, benchi la ufundi na viongozi kwa kuendelea kuutangaza vyema mkoa huo, akiahidi kuwa nao bega kwa bega kwa kila mahitaji yatakayohitajika.

Ushindi wa juzi umeifanya timu hiyo kucheza michezo mitano bila kupoteza, ambapo mara ya mwisho ilichapwa mabao 4-2 na JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Mbweni, Dar es Salaam, Oktoba 18 mwaka huu.

Baada ya hapo ilimtimua kocha, Francis Kimanzi na ikaanza kwa kushinda wa bao 1-0 dhidi ya Pamba Jiji, bao 1-0 dhidi ya Mashujaa FC, ikaitandika Yanga mabao 3-1, ikatoka sare ya bao 2-2 na Singida Black Stars, kabla ya juzi kuitandika KMC nyumbani kwao mabao 2-0.

Ushindi huo umeipeleka Tabora United hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikifikisha pointi 21 katika michezo 13 iliyocheza, ikishinda mechi sita, sare tatu na kupoteza nne.

Kipigo hicho imeifanya KMC kushuka hadi nafasi ya 10 ya msimamo, ikisalia na pointi 14, ikicheza michezo 13, ikishinda nne, sare mbili na kupoteza michezo saba.