WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni amesisitiza Watanzania kuendelea kudumisha amani sambamba na kutumia nyumba za ibada kuhamasisha na kutoa mafundisho ya dini yatakayodumisha amani.
Waziri Masauni aliyasema hayo juzi wakati akifungua Msikiti wa Tawhid eneo la Coco Beach (Zamani Msikiti wa Makuti).
"Tanzania ni nchi ambayo tunavumiliana sana na ndio maana ni rahisi kukuta watu wenye dini tofauti wanaishi kwa upendo, mshikamano bila kubaguana wala kuchukiana,” alisema.
Masauni alisema utamaduni wa kuvumiliana umejengewa misingi imara na waasisi wa taifa.
Alisema ndio maana dini moja huweza kusaidia mchango wa ujenzi nyingine na suala hilo limezidisha amani nchini.
Mwenyekiti wa Taasisi ya The Islamic Foundation, Aref Nahd, alisema kukamilika kwa msikiti huo kutasaidia waumini kutekeleza ibada ya swala tano kwa waislam wanaokwenda katika fukwe hizo kutembea na kupumzika.
Ufunguzi huo pia, ulihudhuriwa na Balozi wa Qatar nchini, Fahad Rashid Al Marekhi, Balozi wa Uturuki nchini, Dk. Mehment Gulluoglu, mashehe na waumini wa dini hiyo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED