Manusura jengo Kariakoo asimulia yaliyomkuta

By Restuta James , Nipashe Jumapili
Published at 01:38 PM Dec 01 2024
Jengo lililoporomoka la biashara Kariakoo.
Picha: Mtandao
Jengo lililoporomoka la biashara Kariakoo.

MANUSURA wa jengo lililoporomoka la biashara Kariakoo, Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu 31 na wengine 88 kujeruhiwa, Kunti Abdallah, amesimulia masahibu yaliyomkuta.

Amesema wakati likiporomoka, alikuwa ndani ya jengo hilo na alianza kufanya maombi akiwa katikati ya vifusi hivyo na kumwezesha kutoka salama.

Mfanyabiashara huyo ambaye ni miongoni waliookolewa baada ya jengo hilo kuporomoka Novemba 16, mwaka huu, ametoa ushuhuda huo juzi katika mkesha wa maombi uliofanyika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kinondoni, Dar es Salaam.

Akishuhudia waumini wenzake, Kunti alisema alikuwa sakafu ya kwanza kati ya tatu zilizokuwa katika jengo hilo.

Alisema akiwa amefunikwa na kifusi, katika hali ya kushangaa, alikumbuka kumwita Yesu, kisha alipata amani kwamba atatoka salama.

“Niliita Yesu mara tatu, nikaanza kusikia maporomoko ya kifusi yakianguka juu ya mwili wangu. Nikasikia uzito na kila kitu kikanielemea.

“Sakafu zote za mizigo zilizokuwa juu yetu, zilituporomokea,” alishuhudia Kunti huku  akibubujikwa na machozi.

Alisema aliendelea kuomba akiwa ndani ya kifusi ilhali amebanwa mwili mzima na baada ya muda, alipata ujasiri wa kufungua macho na kuona nafasi ndogo iliyojitengeneza na kusaidia kumwingizia hewa.

"Nilianza kupata hewa. Nikaanza kumshukuru Mungu na kuimba nikiomba Yesu asinipite. Namshukuru Mungu, walikuja vijana wabeba mizigo ambao waliniambia, walikuta mguu wangu unacheza na walisikia sauti kwa mbali nikiimba.

“Kama si kumwita Yesu, nisingepona. Mimi nilikuwa mwisho kabisa wa jengo,” alisema Kunti aliyeokoka miaka mitatu iliyopita baada ya kubatizwa katika Usharika wa Keko, mkoani humo.

Kunti ni mmoja wa manusura wa ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa tatu lililokuwa mitaa ya Mchikichi na Congo, Kata ya Kariakoo, iliyotokea siku hiyo saa 3:00 asubuhi na kusababisha vifo vya watu 31 na kujeruhi 88.

Tayari wamiliki wa jengo hilo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka 31 ya kuua bila kukusudia.