Yanga, Simba zakwepana Algeria

By Adam Fungamwango , Nipashe Jumapili
Published at 02:20 PM Dec 01 2024
Picha mbili za kuunganisha za mashabiki wa Simba na Yanga.
Picha:Mtandao
Picha mbili za kuunganisha za mashabiki wa Simba na Yanga.

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye mechi za kimataifa, Yanga na Simba zimeonekana kukwepana kwenda pamoja nchini Algeria kwa kutumia ndege moja, baada ya kila mmoja kupanga tarehe tofauti.

Habari zilizopatikana kutoka ndani ya klabu hizo mbili zinasema kuwa kila timu ina itifaki zake, hivyo Yanga imepanga kuondoka Jumanne ijayo, huku Simba ikipanga kuondoka Jumatano zote zikienda nchini Algeria kucheza mechi za kimataifa kwenye miji tofauti.

Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga, inatarajiwa kuondoka Jumanne ijayo na itafikia kwenye mji wa Algiers kucheza mechi ya pili ya Kundi A ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya MC Alger, itakayopigwa Jumamosi ijayo saa 4:00 usiku, Uwanja wa Julliet wa Tano.

"Sisi Mungu akipenda tutaondoka Jumanne kwenda Algeria kwa ajili ya mchezo huo, hatujapanga na mtu, huu ni utaratibu ambao tumeuweka sisi wenyewe," alisema mtoa taarifa kutoka ndani ya klabu ya Yanga.

Simba yenyewe inatarajia kwenda kucheza mchezo wa pili wa makundi wa Kombe la Shirikisho katika Kundi A dhidi ya CS Constantine na inatarajiwa kuondoka nchini Jumatano na kufikia kwenye mji wa Constantine ambako ndiko makao makuu ya timu hiyo.

Mechi hiyo inatarajiwa kuchezwa Jumapili ijayo, saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Mohamed Hamlaoui.

"Nadhani tutaondoka Jumatano kwenda nchini Algeria kwa ajili ya mchezo huo, hatuna taarifa yoyote kwamba eti kuna timu nyingine inabidi tuondoke nayo," kilisema chanzo toka ndani ya klabu ya Simba.

Haya yanakuja kutokana na tetesi na baadhi ya wachambuzi na wadau wa soka kupendekeza kuwa timu hizo zingepewa ndege moja ili kwenda kucheza mechi zao na kusubiriana kwani zote zinakwenda kucheza nchini Algeria.

Wakati huo huo, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema mafanikio yaliyoanza kujitokeza kwenye klabu hiyo yanatokana na uimara wa viongozi wao, wakiongozwa na Mwenyekiti, Murtaza Mangungu.

Alisema kuwa kiongozi huyo alipigwa na mawimbi makali, lakini alisimama imara na kufanya maboresho ndani ya klabu na timu akishirikiana na wenzake, hatimaye leo wanachama na mashabiki wameanza kula mema.

"Mafanikio yaliyoanza kuchomoza sasa ndani ya klabu yetu ni kutokana na uimara wa viongozi wetu wa klabu wakiongozwa na Mwenyekiti wetu Murtaza Mangungu.

Mawimbi makali yalimpiga Mwenyekiti wetu lakini alisimama thabiti na kufanya maboresho ndani ya klabu yetu akishirikiana na viongozi wenzie na hatimaye leo tumeanza kula mema ya Simba

Jukumu letu wana Simba ni kuwaombea viongozi wetu waendelee kuwa madhubuti kwa maslahi ya klabu yetu," alisema Ahmed.