NI bomu jipya kwa maisha ya watu. Hivi ndivyo inavyoweza kuelezwa kutokana na hatari inayoinyemelea jamii kutokana na matumizi ya dawa kwa wanawake hasa wakati wa hedhi.
Matumizi ya dawa za kukata hedhi yameshika kasi mijini hali iliyoamsha wataalamu wa afya na kuonya kwamba zinaweza kusababisha saratani, utasa na kuharibu figo.
Wauzaji katika maduka ya dawa waliozungumza na mwandishi wa habari hii, wametaja wanunuzi ni wenye umri kati ya miaka 17 hadi 35.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hii mkoani Dar es Salaam umebaini kuwa watumiaji wakuu wa dawa hizo ni wanafunzi wa vyuo, wasafiri na kinadada wanaofanya biashara ya kuuza miili yao.
Mfanyakazi wa maduka ya dawa yaliyoko Ubungo, Dar es Salaam, Happy Kasimu, anasema wengi wanaokwenda kununua dawa hizo ni wasichana walio na umri kati ya miaka 17 na 35 hasa wanafunzi wa vyuo na wale wanaofanya biashara ya kuuza miili.
Anasema kwa kuwa duka lake liko karibu na kumbi za starehe ambazo zina wasichana wengi wanaofanya biashara ya ngono, kwa siku huuza dawa hizo kwa watu watatu hadi wanne na wengine anaowafahamu huwatuma bodaboda.
Wakati uuzaji huo wa dawa holela ukifanyika, Novemba, 2023 Waziri wa Afya (wakati huo), Ummy Mwalimu, alitoa onyo kali kwa wafamasia na wamiliki wa maduka ya dawa wanaotoa dawa bila kuangalia cheti cha daktari.
Akifunga Kongamano la Tatu la Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa na kufungua rasmi Wiki ya Uhamasishaji na Uelimishaji Jamii kuhusu matumizi sahihi ya dawa iliyoanza Novemba 18 hadi 24, mwaka jana, Ummy alisema kufanya hivyo ni kuendeleza tatizo la usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa na kuhatarisha afya za watu.
SIMULIZI WATUMIAJI
Doroth Paula, anasema huwa anakunywa vidonge vya kuzuia hedhi pindi anapokuwa safarini kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine. Anasema hufanya hivyo ili kuepuka usumbufu barabarani wa kutafuta sehemu ya kujisitiri au wakati mwingine kuhofia kuchafuka.
“Usumbufu mwingine ni kupata maumivu makali ya tumbo. Safari ndefu halafu njia nzima unaumwa tumbo hata raha ya safari huioni. Unakosa hamu ya kula na matokeo yake ukifika mwisho wa safari unakuwa mgonjwa zaidi. Ndiyo maana natumia dawa ili kuepuka hayo,” anasema.
Moja ya wanaofanya biashara ya kuuza mwili, Rachel James, mwenye miaka 18 (si jina lake halisi), anakiri kutumia dawa aina ya (anaitaja) kukata hedhi endapo anakwenda kukutana na mtu wake anayemwita wa muhimu hasa wale wanaotoa fedha nyingi.
“Mimi siwezi kuacha fedha bora niende duka la dawa nikanunue dawa nikate ili damu ikate niingize mpunga (fedha) na mambo mengine baadaye,” anasema.
Alipoulizwa kuhusu madhara ya dawa hizo, anasema hafahamu kama kuna madhara bali anachojua ni dawa kama dawa zingine.
“Nikiwa katika hedhi biashara yangu ya kuuza mwili, ninapojua ninakutana na mteja wangu wa mara kwa mara huwa nakunywa dawa ili kukata hedhi,” anasema rafiki yake Rachel aliyejitambulisha kwa jina moja la Angel, mwenye miaka 24.
WATAALAM WAONYA
Daktari wa Idara ya Magonjwa ya Wanawake na Uzazi Hospitali ya Aga Khan, Dk. Brenda Ovin, anasema kumeza dawa za kuzuia hedhi (progesterone only pill) au dawa za homoni zinazotumika kuchelewesha au kusimamisha hedhi (norethisterone), huathiri mwili wa mwanamke kwa namna tofauti.
Anasema madhara yanategemea aina ya dawa, muda wa matumizi na hali ya kiafya ya mwanamke, ikiwamo mabadiliko ya mzunguko wa hedhi.
“Dawa zinaweza kubadilisha ratiba ya hedhi, kuifanya ichelewe au isiwe na mtiririko wa kawaida baada ya kusimamisha matumizi,” anasema.
Pia anasema inaweza kusababisha mtumiaji kutokwa na damu isiyo ya kawaida na kwamba baadhi ya wanawake hupata matone ya damu yasiyotarajiwa hata baada ya kutumia dawa hizo na wengine kupata maumivu ya kichwa.
“Kuhisi kichefuchefu au tumbo kujaa ni athari nyingine. Dawa hizi zinaweza kusababisha kichefuchefu kwa baadhi ya watumiaji na kuumwa matiti. Dawa za homoni zinaweza kusababisha matiti kuhisi maumivu au kuvimba kwa muda,” anasema Dk. Ovin.
Anatahadharisha kwamba dawa hizo zinapaswa kutumika tu baada ya kushauriana na daktari ili kuhakikisha zinalingana na hali ya kiafya ya mtumiaji.
Dk. Ovin anasema wanawake wenye matatizo ya kiafya kama shinikizo la damu, kisukari au historia ya saratani ya matiti, wanapaswa kuwa waangalifu zaidi.
“Kama ni muhimu kusimamisha hedhi kwa sababu za kiutendaji, kama safari au hafla, ni bora kutumia dawa hizi mara chache tu na si kwa muda mrefu ili kupunguza madhara yake” anashauri.
Daktari mwingine kutoka Hospitali ya Regency, Dar es Salaam, Geoffrey Stanslaus, anasema kama mtumiaji wa dawa za kuzuia hedhi atatumia kwa muda mrefu, anaweza kuathiri ukuta ambao unatoa damu wakati mwanamke anapokuwa katika hedhi.
Pia anasema inaweza kuvuruga mzunguko wa homoni, jambo litakalosababisha kuona mzunguko wa hedhi katika siku tofauti.
Dk. Stanslaus anasema wale wanaofanya tabia hiyo, ukubwani wanaweza kupata saratani inayoanzia katika ukuta wa uzazi. Anasema mfumo wa homoni ukishavurugika unaweza kumsababishia kuongezeka siku za hedhi na kujiweka katika hatari ya kutoshika mimba.
Kuhusu matatizo mengine nje na hayo, anasema jambo hilo ni jipya bado halijafanyiwa utafiti ili kubaini madhara mengine makubwa zaidi ya hayo.
Mtaalam huyo anasema wako wagonjwa wanaokwenda kupatiwa matibabu hospitalini hapo, ambapo sio rahisi moja kwa moja kutambua kwamba sababu ni matumizi ya dawa hizo mpaka mgonjwa mwenyewe asimulie.
Dk. Stanslaus anasema katika uchunguzi wake, wengi wanaofanya hivyo huwa wanakuwa na dharura kama mitihani, harusi na wengine huwa ni tabia za kihuni ili akutane na mtu wake.
Daktari kutoka Hospitali ya Mnazi Mmoja, Nashie Shongopa, anasema tabia ya kunywa dawa za kusitisha hedhi zinasababisha msongo wa mawazo kwa mhusika baadaye.
“Kama hajapima kujua homoni zake zipoje halafu anakunywa dawa hizo ambazo zinaongeza homoni, itamuwiya vigumu kupata ujauzito baadaye na hiyo itamfanya kuwa na msongo wa mawazo,” anasema.
Mtaalam huyo anasema matumizi holela ya dawa bila kufuata ushauri wa mtaalam humweka mtu katika hatari ya kupata tatizo la figo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED